http://www.swahilihub.com/image/view/-/4895246/medRes/2197886/-/1a5ce5z/-/wangari.jpg

 

Nadharia anuwai katika uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  12:20

Kwa Muhtasari

Baadhi ya wasomi wanasema nadharia za kuhakiki vilevile huathiriana sana.

 

WASOMI tajika mathalani kina Wellek wanaeleza kwamba nadharia za kuhakiki vilevile huathiriana sana.

Kwa mintarafu hii, huwa ni vigumu kuongea kuhusu swala la ubunifu katika nadharia yoyote ya kuhakiki.

Isitoshe, nadharia hizi zimegawika katika makundi mengi kutegemea malengo na mbinu zake.

Kuna nadharia tofautitofauti jinsi zilivyoainishwa katika vitengo vifuatavyo:

i. Nadharia zinazomulika maswala bia ya kiulimwengu yanayotokeza katika fasihi

ii. Nadharia zinazohusiana na saikolojia kama vile saikolojia changanuzi

iii. Nadharia zinazohusiana na visasili

iv. Nadharia zinazojihusisha na maswala ya jamii

v. Nadharia za umuundo wa fasihi na nyinginezo

Tutaziangazia baadhi ya nadharia hizo anuai kwa njia ifuatayo:

Nadharia ya Ufeministi

Ufeministi ni dhana inayotokana na neno la kilatini 'femina' linalomaanisha mwanamke.

Kwa mantiki hii dhana ya ufeministi inarejelea uwakilishaji wa haki za wanawake kufuatana na imani ya usawa wa kijinsia.

Nadharia hii imejikita sana katika mwamko wa wanawake unaolenga kupigania na kukomesha udhalimu dhidi yao na kufichua matatizo wanayoyapitia katika jamii.

Mwalimu Mbatiah (2001), anaeleza kuwa Ufeministi ni nadharia ya fasihi ambayo inajishughulisha na utetezi wa haki za wanawake dhidi ya ugandamizwaji katika jamii yenye mfumo uliodhibitiwa na wanaume - yaani mfumoume.

Kulingana na mawazo yake, nadharia imedhamiria kuupigania ukombozi wa mwanamke kutokana na pingu za kitamaduni, kiuchumi, kidini, kijamii na kisiasa. Pingu anazozirejelea ni misimamo ya itikadi ya kiume ya ubabedume.

Mawimbi ya kifeministi

Mawimbi ya kifeministi yalianza kuvuma ulimwenguni katika karne ya kumi na tisa na yakashika kasi miaka ya sitini na sabini ya karne ya ishirini.

Kwa upande wake Ntarangwi (2004), nadharia ya Ufeministi iliibuka katika muungano wa ukombozi wa wanawake uliopamba moto katika miaka ya sitini huko Marekani.

Wakati huo, wanawake hasa wa Kimagharibi walianza kuzungumzia matatizo yao kwa kuyaandika.

Kwa uwazi na ubayana maswala ya kifeministi yalishika mizizi miaka ya sitini.

Jinsi anavyotongoa Bonny Onyoni (2002), kulikuwa na jitihada mbalimbali za kupigania usawa baina ya wanaume na wanawake ingawa hazikuchapishwa.

Kwa mfano, katika nchi ya Ufaransa kuanzia mwaka 1789 hadi mwaka 1795, inadaiwa kulikuwa na maandamano ya wanawake kupinga kudunishwa; ni kitu walichokiita 'Msimbo wa Napoleon.’

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo:

Mulokozi, Mugyabuso & Kahigi K. (1979). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.

Njogu, K. & R.M. Wafula (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Shihabuddin, C. (1970). Utangulizi: Malenga wa Mvita. Nairobi: Oxford University Press.