Nadharia mbalimbali kuhusu chimbuko la Sheng

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Saturday, August 5  2017 at  15:36

Kwa Mukhtasari

Wachunguzi wengi wanakubaliana kuwa Sheng ilizuka katika miaka ya katikati ya sitini na sabini katika sehemu za makazi eneo la Mashariki mwa Nairobi kama vile vitongoji duni vya Kaloleni, Mbotela, Kimathi, Pumwani, Majengo, Bahati, Buruburu, Barma, Umoja, Dandora, Huruma, Mathare, Eastleigh na viunga vyake kulingana na Mbaabu na Nzunga, (2003).

 

KATIKA makala ya awali tuliangazia mada kuhusu suala la lugha huku tukirejelea msimbo wa sheng.

Tulitathmini Sheng kama tukio la kijamii ambapo tuliona kuwa msimbo huu hutumika mno miongoni mwa vijana kwa madhumuni ya kujitambulisha kama kundi la kijamii maoni yanayotiliwa mkonde na Shitemi.

Aidha, wachunguzi wengi wanakubaliana kuwa Sheng ilizuka katika miaka ya katikati ya sitini na sabini katika sehemu za makazi eneo la Mashariki mwa Nairobi kama vile vitongoji duni vya Kaloleni, Mbotela, Kimathi, Pumwani, Majengo, Bahati, Buruburu, Barma, Umoja, Dandora, Huruma, Mathare, Eastleigh na viunga vyake kulingana na Mbaabu na Nzunga, (2003).

Kufikia miaka ya awali ya 1970, Sheng ilikuwa imepamba moto sio tu Nairobi bali pia katika miji mingine kote nchini Kenya. Kwa sasa, Sheng imekuwa kitambulisho cha takriban vijana  wote nchini, mijini na mashambani wawe wa shule au la.

Mukhebi (1986: 11) anasema Sheng ni tukio la kitamaduni ambalo linafungamana sana na mawazo au fikira, hisia na matakwa ya watumiaji wake.

Anaeleza kuwa wazungumzaji asilia wa Sheng waligundua kuwa kutokana na hali na mazingira yao ya kifukara katika mitaa ya jamii yenye mapato ya chini, hawangeweza kupata elimu yao na kuwasiliana kupitia Kiingereza bali walihitaji mfumo wao wenyewe.

Anaeleza pia kuwa kutokana na ufahamu wao duni wa Kiingereza, iliwawia vigumu vijana hao kuweza kujifunza masomo mseto kwa Kiingereza kama vile Historia, Jiografia, Fasihi na maisha ya kijamii ya Waingereza, masomo yaliyokuwa ya kimsingi katika mitala ya shule za msingi wakati huo.

Nini hasa chimbuko la Sheng?

Kuna nadharia mbalimbali zinazojaribu kueleza asili na chimbuko la Sheng. Hata hivyo, kuan nadharia kuu mbili zilizokita mizizi kama ifuatavyo:

  • Nadharia ya uhuni

  • Nadharia ya msimbo wa vijana

 

NADHARIA YA UHUNI

Kwa mujibu wa nadharia ya uhuni, msimbo wa Sheng ulibuniwa na kuibuka kutokana na wahuni au wakora jijini Nairobi anavyosema Kobia, (2006).

Waliunda baadhi ya maneno kutoka nyuma kuelekea mbele badala ya muundo wa kawaida wa neno.

Kwa mfano, neno kama ‘nyama’ lilibuniwa na kuwa ‘manya’.

Kwa mukhtasari, nadharia ya uhuni inahusisha kubuniwa kwa Sheng na haja ya wahuni kuwasiliana kwa ‘lugha’ ambayo watu wengine hawangeweza kuifahamu.

Mazrui (1995) anadai kwamba Sheng iliibuka miaka ya thelathini jijini Nairobi kama lugha ya wahuni. Ilikuwa ‘lugha’ ya wahuni ya kujitambulisha hasa wale wanaonyakua mali za watu na kutoroka.

 

NADHARIA YA MSIMBO WA VIJANA

Hii ni nadharia inayodai kwa upande mwingine kuwa Sheng iliibuka katika mitaa ya mashariki mwa Nairobi mnamo miaka ya sabini kulingana na Osinde, (1986); Shitemi, (2001).

Kufuatia kupatikana kwa uhuru hapo mwaka wa 1963, idadi ya wakazi wa jiji la Nairobi ilipanda kwa haraka sana kutokana na kumiminika kwa watu kutoka mashambani wakitafuta nafasi za kazi katika mitaa ya viwanda humo jijini.

Wananchi hao maskini waliishia kuishi katika mitaa ya makazi duni ya viwandani mashariki mwa Nairobi ambapo ndicho kitovu cha maendeleo ya viwanda.

Ijapokuwa wafanyikazi hawa pamoja na jamii zao walilazimika kutumia Kiswahili kwa mawasiliano baina yao, wengi walikichukia Kiswahili kwa vile kilikuwa kimedunishwa sana na sera ya ukoloni kama lugha ya mashambani, lugha ya vibarua au “maboi” wa kuwatumikia Wazungu.

Hata hivyo, watoto wa wafanyikazi hao hawakupendelea kuendelea kukitumia Kiswahili kama wazazi wao kwa sababu kadha kama zifuatazo:

Kwanza kabisa kinyume na wazazi wao, watoto wale walilazimika kuishi katika hali ya jamii ya utatu-lugha: lugha za kinyumbani, Kiswah

ili na Kiingereza.

Vilevile walitambua kuwa ingawa walilazimika kutumia lugha nyingi, ni Kiingereza pekee ambacho kilipewa hadhi ya juu kama lugha ya utawala, mamlaka, heshima na uwezo wa kiuchumi.

Ili kuepuka matatizo ya kimawasiliano na kama njia ya kusuluhisha utata wa hali hiyo iliyowakabili, vijana hao waligundua msimbo wa mawasiliano kati yao ambao, ingawa ulifuata sarufi ya Kiswahili, uliazima msamiati kutokana na lugha za kiasili na kuunda baadhi ya maneno yake.

Sheng ndivyo ilivyochipuka na kuendelea hadi ilivyo katika kizazi cha leo.

 

Marejeo:

Kobia, J. 2006. Sheng is not a language but a popular slang

Lo Liyong, T. 1972. The Popular Culture of East Africa. Nairobi: Longman.

Mazrui, A. na Mazrui, A. 1995. Swahili, State and Society. Nairobi: EAEP

Una swali? Muulize mwandishi kupitia anwani: marya.wangari@gmail.com