http://www.swahilihub.com/image/view/-/4864754/medRes/2178260/-/bl8iwsz/-/mwambao.jpg

 

Nadharia za chimbuko la Kiswahili (Sehemu ya Pili)

Unguja

Mwambao wa Pwani, Unguja. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Friday, November 23  2018 at  07:09

Kwa Muhtasari

Tunajadili nadharia ya lugha mseto na nadharia kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu.

 

NADHARIA YA LUGHA MSETO AU LUGHA CHOTARA

Baadhi ya watu wanaoshikilia kuwa Kiswahili ni lugha ya mseto ni pamoja na Fredrick Johnson, Carl Meinhof, G.W. Broomfield, W.E. Taylor, Askofu Dakta Steere, W. Broomfield, W.H. Whiteley miongoni mwa wengine.

Kwa mujibu wa nadharia hii kuingiliana kwa lugha za kigeni kama vile Kiarabu, Kiajemi, Kihindi na lugha za makabila ya wenyeji wa pwani ya Afrika Mashariki, maneno yalichukuliwa na vizalia vya mazingira hayo ya maingiliano kutoka kwa lugha hizo.

Aidha, nadharia hii inadai kuwa wageni walioana na wenyeji na kwa hivyo lugha zao za akina baba, mama na wajomba zilitumiwa kuunda lugha ya Kiswahili.

Isitoshe, wanadai Kiswahili kilizuka ili kufanikisha mawasiliano katika shughuli za kibiashara na kwamba hakikuwepo kabla ya kuja kwa wageni.

 

Udhaifu wa Nadharia ya Lugha Chotara

Madai haya ya lugha mseto vilevile hayana msingi. Kulingana na taaluma ya isimu, lugha chotara au pijini huwa tofauti sana na lugha zinazokutana au kuchanganyana ili kuibusha. Uchanganuzi wa lugha ya Kiswahili unaonyesha ni lugha yenye tabia na sifa za Kibantu.

Udhaifu mwingine wa nadharia hii ni kuwa inaegemea kwenye kipimo au kigezo kimoja tu: msamiati.

Ni ukweli kuwa Kiswahili kina maneno mengi ya Kiarabu, Kiajemi, Kihindi, Kireno, Kiingereza lakini kigezo cha msamiati pekee hakitoshi. Lazima muundo na sifa nyinginezo kama sauti uchunguzwe.

NADHARIA KUWA KISWAHILI NI LUGHA YA KIBANTU

Huu ndiyo msimamo unaokubaliwa na watu wengi. Mwasisi wa nadharia hii alikuwa Profesa Malcolm Guthrie.

Wataalamu wanadhihirisha kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu kwa kufafanua awamu zifuatazo za maenezi ya Wabantu.

Kulingana na utafiti wa wataalamu hawa, chimbuko la Wabantu ni Afrika Magharibi, sehemu za nchi ya Kameruni. Kutoka huko, Wabantu walienea katika sehemu wanazokalia sasa. Maenezi haya yalifanyika katika awamu mbalimbali katika kipindi kirefu.

Awamu ya kwanza kulingana na ushahidi wa kihistoria ilifanyika kati ya mwaka 40 hadi 10 Kabla ya Kristo (KK).

Mtandao huu wa maenezi ulilipeleka kundi moja la Wabantu hadi ukanda wa Kusini mwa misitu ya Kongo na kundi jingine sehemu za Magharibi ya eneo la Ziwa Viktoria.