http://www.swahilihub.com/image/view/-/4863346/medRes/2124995/-/103tibu/-/usailko.jpg

 

Nadharia ya Maumbile ya Mwanadamu

Usaili wa ajira

Lugha ni muhimu katika mawasiliano ya wanadamu. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Thursday, November 22  2018 at  10:03

Kwa Muhtasari

Kufikiria kwa urazimu ni mojawapo ya sifa za binadamu ambazo wanyama wengine hawana.

 

KATIKA makala iliyotangulia, tulichambua nadharia ya mchangamano wa mahusiano ya kijamii kuhusiana na chimbuko la lugha.

Kwa mujibu wa nadharia hii ni bayana wanadamu ni lazima waliishi katika makundi ya kijamii, na iwapo tunaafikiana kuhusu hayo, ni lazima tukubali kwamba yamkini kulikuwa na kanuni maalumu ambazo zilitawala mfumo wao wa mawasiliano katika maisha yao na mahusiano yao ya kijamii.

Halkadhalika, nadharia hii bado inakosa majibu ya swali nyeti kuhusu asili ya hizo sauti zilizozalishwa.

Ikiwa chanzo cha lugha ni mahusiano ya kijamii, kuna wanyama wengine wanaoishi katika makundi makundi mathalani tumbili na ngedere lakini mawasiliano haya hayaendelei na kubadilika kuwa matamshi ya lugha.

NADHARIA YA MAUMBILE YA MWANADAMU

Badala ya kuchunguza asili ya sauti za mwanadamu na kuibua dhana kuwa huenda ndizo chanzo na asili ya lugha ya mwanadamu, ni vyema kuangazia sifa za kimaumbile alizo nazo mwanadamu.

Yule (2010) anafafanua kwamba uchunguzi huu unajikita katika zile sifa ambazo viumbe wengine (wanyama) hawana.

Msimamo wa nadharia hii ni kuwa tofauti ya kimaumbile kati ya mwananadamu na wanyama kama nyani ndiyo iliyokuwa chanzo cha lugha ya mwanadamu.

Pizarro na Bloom (2003) wanataja sifa ya kufikiria kwa urazimu (conscious reasoning).

ISIMU

Wataalamu wengi wa lugha yamkini wanaafikiana na fasili kwamba isimu ni elimu ya sayansi ya lugha.

Aidha, isimu inaweza kufafanuliwa kama uchunguzi wa kisayansi na wa kimantiki kuhusu vipengele na sifa mbalimbali za lugha.

 

Kwa nini Isimu ni Sayansi?

Kwa mujibu wa Verma et al (1989), isimu ni "sayansi kwa kuwa hufuata na kutumia mbinu za kimsingi za utafiti wa kisayansi" (uk. 29).

Mbinu hizo ni kama zifuatazo:

 1. Uchunguzi uliodhibitiwa

 2. Uundaji wa mabunio

 3. Uchanganuzi

 4. Ujumlishi/ujumuishi

 5. Utabiri

 

Upeo wa Isimu

Jinsi wanavyosema Habwe na Karanja(2003). katika kushughulikia lugha wanaisimu hujaribu kujibu maswali kama yafuatayo:

 1. Lugha ni nini?

 2. Asili ya lugha ni nipi?

 3. Lugha hufanya kazi namna gani katika mawasiliano?

 4. Lugha inahusiana namnagani na asasi nyingine maishani?

 5. Kujua lugha ni nini?

 6. Namna gani mtoto anajifunza lugha?

 7. Kwa nini lugha hubadilika?

 8. Lugha zinatofautiana kwa kiasi gani?

 

Marejeo

Cook, J. (1969), 'The analogy between first and second language learning', International  Review of Applied Linguistics, VII/3, 207-216

Habwe, J., na Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.