Nadharia ya mawasiliano ikiwemo mabadiliko katika mawasiliano

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Wednesday, October 31  2018 at  11:30

Kwa Muhtasari

Zipo nguzo muhimu za nadharia ya mawasiliano.

 

NGUZO au mihimili ya Nadharia ya Mawasiliano ni kama ifuatavyo:-

  1. Kanuni za kisarufi na mbinu nyinginezo zinatumiwa inapoonekana kuwa ni lazima.
  2. Wanafunzi wanaweza kuzungumza kuanzia siku ya kwanza.
  3. Lugha ya kwanza na tafsiri zinaweza kutumiwa ikiwa hapana budi, pale matumizi yake yanaposaidia ufafanuzi wa jambo.
  4. Kusoma na kuandika kunaweza kuanza katika siku za mwanzo ikiwa ni muhimu.
  5. Matumizi ya lugha kwa wingi darasani hupendekezwa kwani nadharia hii husisitiza kuwa mtu hujifunza lugha vizuri kwa kuitumia.
  6. Jukumu muhimu la ujifunzaji wa lugha ni mawasiliano yanayofaa katika muktadha.

Nadharia ya mawasiliano inapendekeza ufundishaji ambao unatumia shughuli zinazoendeleza mawasiliano.

Hii ni kwa sababu waasisi wa nadharia hii wanaamini kuwa ujifunzaji wa lugha huendelezwa na vitendo au shughuli zinazoendeleza mawasiliano badala ya ukaririshaji wa miundo.

Vitendo mathalan ulinganishaji wa picha, maelezo yanayohusu ramani, maelezo ya ufanyaji wa shughuli fulani kwa mfano, kupika chakula fulani, kuonyesha njia, mazungumzo ya vikundi, tamthilia fupi, uigizaji, michezo, mijadala na usomaji wa magazeti hupendekezwa darasani.

Katika darasa la aina hii, mwalimu huchukuliwa kama mratibu wa shughuli hiyo. Kazi yake muhimu huwa ni kuwezesha mawasiliano kuwapo kati ya wanafunzi darasani. Mwalimu pia huwapa wanafunzi ushauri ufaao.

Ni muhimu kuelewa kwamba darasa linalotumia nadharia ya mawasiliano hushirikisha wanafunzi sana katika mawasiliano. Mwalimu haachiwi jukumu lote la kusema na kutenda. Jukumu lake huwa limebanwa kidogo. Wanafunzi huhimizwa kufanya mengi darasani.

MABADILIKO KATIKA MAWASILIANO

Mawasiliano yanazidi kubadilika kadri na mpito wa wakati kutokana na mabadiliko na ukuaji wa teknolojia ambao umeibua mawazo mapya kuhusu mawasiliano.

Kwa mujibu wa watafiti, mabadiliko katika mawasiliano yanaweza kuangaziwa katika hatua tatu.

Mabadiliko ya mwanzo: mawasiliano ya kwanza katika maandishi yalianza na michoro. Maandishi hayo yaliyoandikwa kwenye mawe yalikuwa mazito kuhamishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine

Enzi hizo mawasiliano ya maandishi hayangeweza kubebwa, ingawa yalikuwepo.

Mabadiliko ya pili: maandishi yalianza kufanyiwa katika karatasi, nta, udongo na kadhalika. Aidha, herufi za alfabeti zilibuniwa hivyo kuwezesha mfanano wa lugha katika maeneo makubwa.

Baada ya muda, shirika la uchapishaji la Gutenberg lilianzishwa.

Shirika hili lilitayarisha kitabu cha kwanza cha kuchapishwa likitumia mashine yake na kitabu hicho kilikuwa Biblia.

Maandiko hayo yaliweza kusafirishwa kwa watu wengine ulimwenguni ili wayaone na yaliweza kuhifadhiwa na hata kubebwa.

Mwandishi anapatikana kwa baruapepe: marya.wangari@gmail.com

 

MAREJEO

Mehrabian na Ferris (1967). "Inference of Attitude from Nonverbal Communication in Two Channels". Katika: The Journal of Counselling Psychology Vol.31, 1967, pp.248-52

Witzany, G. (2006 Plant Communication from Biosemiotic Perspective. Plant Signaling na Behavior 1 (4): 169-178

Witzany, G. (2007 Applied Biosemiotics: Fungal meddelande. Katika: Witzany, G. (Ed). Biosemiotics in Transdisciplinary Contexts. Helsingfors, Umweb, uk. 295-301