Nadharia ya tendo uneni

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Thursday, November 23  2017 at  07:38

Kwa Mukhtasari

Nadharia ya tendo uneni hudai kuwa viambo vya lugha vina uwezo wa kutenda aina fulani fulani ya matendo ya kimawasiliano mathalan kuelekeza, kuahidi, kuomba radhi na kadhalika.

 

NADHARIA ya tendo uneni hudai kuwa viambo vya lugha vina uwezo wa kutenda aina fulani fulani ya matendo ya kimawasiliano mathalan kuelekeza, kuahidi, kuomba radhi na kadhalika.

Unenaji wa viambo hivyo ndio utendaji wa matendo yanayodokezwa na vitenzi husika katika viambo hivyo.

Kila kinachotendwa kwa kunena tu au kutoa tu semo fulani ndicho huitwa tendo uneni.

Masharti ya Tendo Uneni

Kwa mujibu wa Austin,matendo uneni hayakamiliki kwa sababu tu vitenzi tendeshi vimetumika.

Kuna masharti ya uneni ambayo lazima yatimizwe ndipo tendo uneno husika likamilike.

Anabainisha masharti sita na kuyagawa katika makundi matatu (A, B na C)

Kundi A

Lazima kuwe na utaratibu kaida (ambao unatambulika ulimwengu mzima - universal) juu ya utendaji wa tendo hilo na kwamba athari ya tendo hilo ijulikane mahali pote.

Mazingira na watu wanaohusika katika uneni wa tendo husika lazima yawe mwafaka

Kundi B

Utaratibu wa kutenda au kutekeleza tendo husika lazima ufuatwe kwa usahihi.

Utaratibu huo lazima pia ufuatwe kikamilifu.

Kundi C

Aghalabu wahusika wawe na mawazo huria na dhamira ya kweli ya kufanikisha tendo husika.

Iwapo shughuli au wajibu ambao anatakiwa kutimiza baada ya tendo uneno unafahamika basi ni lazima wahusika watekeleze.

Hali maridhawa katika matendo uneni

Austin anafafanua kuwa ili tendo uneni likamilike na kukubalika ni lazima kuwe na kile alichokiita hali maridhawa kinachohalalisha tendo husika.

Hali maridhawa ni jumla ya vitendo na sifa ambazo tendo uneni husika huhitaji ili kukidhimau ili liwe halali au litimie.

Kwa kiasi kikubwa hali maridhawa imetokezwa katika sifa ya matendo uneni.

Viambajengo vya hali maridhawa

Hali maridhawa inahusu mambo yafuatayo:

Nani anayeongea/nena/uliza/ au anayetenda tendo uneni.

i. Ananena nini

ii. Anasema kwa nani/anamnenea nani?

iii. Ananena wapi 

iv. Ananena kwa sababu/lengo gani?

Kwa mfano: Wewe ni nani unayenihukumu miaka 20 jela? Wewe ni nani unayenibatiza?

Miundo ya matendo uneni

Ili kujua vizuri miundo ya matendo uneni ni muhimu kukumbuka uainishaji wa sentensi uliofanywa na wanafalsafa mantiki ambapo wanafalsafa hao walizigawa katika makundi matatu; Maelezo, Maelekezo na Swali.

Miundo ya matendo uneni hupatikana kwa kuangalia kiwima au kiukinzani kati ya sentensi na dhima ambayo sentensi hiyo inakumbatiwa/kuibeba.

Miundo hii iko kama ifuatavyo:-

1. Matendo Uneni Dhahiri

Haya ni matendo uneni ambayo huonyesha kiwima kati ya aina ya sentensi na dhima ambayo inabeba.

Marejeo

1. Massamba P. B. D (2004) Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.

2. Mdee, J. S (1997), Nadharia na Historia ya Leksikografia, Dar es Salaam:TUKI.

3. Morris, Charles W. (1971), Writings on the general theory of signs, The Hague: Mouton