Nadharia za chimbuko la lugha

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Wednesday, November 21  2018 at  13:49

Kwa Muhtasari

Zipo nadharia za kuelezea chimbuko la lugha ingawa wanaisimu hawajawahi kuafikiana kuhusu asili ya lugha.

 

KATIKA makala iliyopita tuliangazia kuhusu nadharia ya mtazamo wa kidini au uungu katika chimbuko la lugha ya binadamu.

Suala la msingi katika nadharia ya kiungu ni kwamba lugha za mwanadamu zina asili moja na ndio maana wanaisimu wa kisasa wamekuwa wakizungumza kuhusu suala la sarufi bia.

Udhaifu wa Nadharia ya Kiungu/ Mtazamo wa kidini

Udhaifu wa nadharia ya kiungu ni kwamba zinashindwa kujibu swali kama vile: Kwa nini lugha nyingine zinazuka tu siku hizi bila ya kuwa nazo zimetoka kwa Mungu?

Aidha, mtazamo huu haujajikita katika tafiti za sayansi ya lugha yaani Isimu na vilevile nadharia hii  haijafuata taratibu za kiuchunguzi wa kiisimu ambayo ndio sayansi ya lugha.

NADHARIA YA WIGO WA SAUTI  ZA ASILI/ CHANZO ASILIA

Yule (2010), anasema nadharia ya wigo sauti inashikilia msimamo kuwa sauti za awali kabisa za lugha ya binadamu ni matokeo ya binadamu kuiga sauti asilia ambazo wanawake na na wanaume walizisikia katika mazingira yao.

Aidha, nadharia hii inaungwa mkono na baadhi ya maneno ambayo yanatokana na sauti asilia za milio ya vitu kama vile vitu vinapodondoka, au kugongana ambayo huitwa onomatopoeia.

Licha ya uthibitisho unaoweza kutolewa kwa maneno hayo machache ambayo huenda kila lugha inayo, nadharia hii ina udhaifu wake jinsi ifuatavyo:

Udhaifu wa nadharia ya Wigo wa Sauti Asili/ Chanzo Asilia

Nadharia hii haijitoshelezi kwa kuwa kuna maneno mengi tu ambayo kwa asili yake hayatokani na milio ya vitu, kama vile majina, na vitenzi ambayo ni matokeo ya njia nyingine za uundaji wa maneno na wala sio uigo wa sauti asilia.

NADHARIA YA MCHANGAMANO WA MAHUSIANO YA KIJAMII

Nadharia hii inatokana na dhana kwamba binadamu wakati fulani katika maisha yake alihitaji msaada wa mwanadamu mwingine katika kufanya kazi.

Katika kazi hizo binadamu hao walitoa milio na sauti mbalimbali za kuhamasishana.

Ni kutokana na sauti hizo ambapo inasemekana ndipo lugha ilipoanza.

Hata hivyo wazo la kimsingi la nadharia hii ni kwamba maendeleo ya lugha ya mwanadamu yanatokana na mazingira ya kijamii alimoishi mwanadamu.

Marejeo:

Cook, V.J. (1969), 'The analogy between first and second language learning', International  Review of Applied Linguistics, VII/3, 207-216

Habwe, J na Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers