Nafasi ya vikoa vya maana katika mawasiliano

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  13:19

Kwa Muhtasari

Maneno katika kitengo kimoja yanaweza kuhusiana kwa namna mbalimbali.

 

JINSI tulivyofafanua awali, vikoa vya maana ni seti ya kuonyesha uhusiano kimaana. Maneno katika kitengo kimoja yanaweza kuhusiana kwa namna mbalimbali, kwa mfano:

  1. Unyume
  2. Usinonimia
  3. Uhiponimi
  4. Umeronimia na kadhalika

Kwa maana nyingine, uhusiano huu ni wa kifahiwa.

Jinsi usinonimia unaweza kutumika kueleza maana ya maana

Kwa mfano mtu mmoja labda hajui maana yawadhifa-ili kumsaidia utamwambia cheo- hapa utakuwa umetumia ujuzi wa sinonimia katika kuelezea maana ya maana. Au unaweza kumweleza mtu maana ya neno kwa kumweleza kinyume chake. Kwa mfano anataka kujua nadra unamweleza kinyume chake tu.

Sifa ya vikoa vya maana

Hakuna sifa maalumu katika kuanza. Unaweza kuanza na neno lolote. Kwa mfano, nikitaka kusema wanyama: naweza kuanza na neno lolote kama vile simba na kadhalika.

Umuhimu wa vikoa vya maana

i. Husaidia kujua maana ya maneno katika lugha. Kwa mfano ili uweze kujua kikoa cha wanyama lazima ujue baadhi ya wanyama

ii. Husaidia katika kujifunza lugha. Kwa mfano mtoto anapojifunza rangi huanza na kikoa cha rangi nyeupe na nyeusi.

iii. Vikoa vya maana husaidia kuchanuza maana katika lugha

iv. Husaidia kuonyesha umbo la wingi. Kwa mfano badala ya kusema kikoa cha tunda tunasema kikoa cha matunda- yaani umbo la wingi ni la msingi sana katika vikoa vya maana.

v. Hurahisisha mawasiliano au huokoa muda. Kwa mfano ukifika sokoni unaweza

vi. Kusema Je, kuna mboga za majani? yaani badala ya kuuliza iwapo kuna mchicha, kunde sukuma wiki na kadhalika.

vii. Hufanikisha shughuli za wanafunzi wa leksikografia

Changamoto ya Vikoa vya Maana katika Kufafanua Semantiki

i. Kuna baadhi ya vikoa ambavyo havina idadi maalumu kwa mfano; idadi ya siku za wiki, wanyama na kadhalika.

ii. Baadhi ya vikoa vya maana memba zake wana uhusiano wa karibu sana kiasi kwamba ni vigumu sana kuelewa. Kwa mfano chui na dubu

iii. Dhana hizi ziko akilini mwa watu tu.

Marejeo

Massamba P. B. D (2004) Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.

Mdee, J. S (1997), Nadharia na Historia ya Leksikografia, Dar es Salaam: TUKI.

Morris, Charles W. (1971), Writings on the general theory of signs, The Hague: Mouton