Nafasi ya wanawake katika Kigogo

Na PHYLLIS MWACHILUMO

Imepakiwa - Thursday, April 12  2018 at  15:03

Kwa Muhtasari

Asiya ni muuza pombe haramu ambayo inawadhuru vijana ila yeye hajali hayo.

 

KATIKA tamthilia ya Kigogo (Pauline Keya), wanawake wana majukumu muhimu kama ilivyo katika jamii halisi. Kunao wahusika wengi wanawake wanaoitawala tamthilia. Pengine hali hii inaandamana na kuwa mwandishi wake ni mwanamke.

Baadhi ya hao ni Shujaa Tunu ambaye anawaongoza Wanasagamoyo kudai haki zao na kumuondoa kiongozi dhalimu mamlakani.

Huyu Tunu ni msomi wa uanasheria hivyo basi anao uelewa unaomfaa katika kutekeleza majukumu haya. Mamake Tunu, Bi Hashima, anamuunga mkono bintiye katika vita hivi.

Hata hivyo, kunao wanawake ambao wanaonekana kuwa wabinafsi sana na wenye kujitakia makuu. Hawa ni Husda na Asiya. Husda ni mke wa kiongozi Majoka ambaye bila shaka aliolewa naye Majoka ili afaidi mali haramu ya kiongozi huyo. Vilevile anasawiriwa kuwa mkware kutokana na jinsi anavyozungumza kwa simu na watu wengine.

Asiya ni muuza pombe haramu ambayo inawadhuru vijana ila yeye hajali hayo. Yeye ni mke wa Boza ila anaendeleza uhusiano wa kimapenzi na Ngurumo, kibaraka wa Majoka, ili apate kandarasi ya kupika keki za uhuru. Asiya anajitihada nyingi ilmuradi apate pesa bila kujali zinatoka wapi. Hawa wanawake wawili bila shaka wanauonyesha upungufu mkubwa walio nao nao wanawake.

Wanawake kama vile Ashua wanatumika kuonyesha pande mbili za hisia za wanawake. Moja ya pande hizo ni kuwa mama mwenye huruma na mke mwema. Ashua anayajali maslahi ya wanawe kiasi cha kujihatarisha kwa kwenda kwa Majoka kumtaka msaada.

Katika hali hiyo, anaonyesha ujasiri mkubwa anapoenda kukutana ana kwa ana na Majoka kumuomba msaada licha ya kuwa yeye ni mke wa Sudi. Hata hivyo, inaonekana kuwa yeye bado ana matamanio ya kupata mali na maisha mema kuliko aliyokuwa nayo wakati huo.

Inaonekana pia kuwa Ashua ni mwerevu sana kwa kuwa anajifanya kuwa amemkana Sudi ili kujiokoa yeye na wanawe kutokana na udhalimu wa Majoka. Yote haya yanatupatia sura kamili ya mahangaiko ya wanawake mbalimbali katika jamii yao na jinsi wanavyoielekeza.