Mchango wa wanafalsafa katika taaluma ya Pragmatiki

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Friday, November 10  2017 at  14:20

Kwa Mukhtasari

Taaluma ya pragmatiki kwa kiasi kikubwa imeimarishwa na kuathiriwa kwa kina na wanafalsafa zaidi kuliko wanaisimu.

 

TAALUMA ya pragmatiki kwa kiasi kikubwa imeimarishwa na kuathiriwa kwa kina na wanafalsafa zaidi kuliko wanaisimu.

Jambo hili limeibua mjadala miongoni mwa baadhi ya wataalamu kuhusu iwapo pragmatiki ni taaluma ya isimu au ya falsafa.

Wanafalsafa waliotoa mchango katika pragmatiki wapo katika makundi mawili:-

  1. Wanafalsafa Mantiki na Masharti-Ukweli (Alfred Tarski)
  2. Wanafalsafa wa Lugha ya Kawaida

Wanafalsafa Mantiki na Masharti-Ukweli (Alfred Tarski)

Kundi hili lilikuwa na madai kadha jinsi tutakavyoyafafanua.

Wao waliona kuwa kuna aina kuu tatu za sentensi;

Sentensi Maelezo, Sentensi Maelekezo na Sentensi Maswali.

Kila aina ya sentensi katika makundi haya matatu ina dhima yake maalum au msingi kama ifuatavyo:-

Sentensi ya maelezo hutumika kutoa taarifa fulani au kueleza wazo.

Sentensi ya maelekezo hutumika kumtaka mtu atende jambo kama alivyoelekezwa na msemaji na hapa kuna sentensi za maombi na amri

Sentensi ya maswali hutumika kuhoji mambo ili kupata ufafanuzi wa jambo fulani.

Wanafalsafa wa Lugha ya Kawaida

Kundi hili liliibuka kupinga hoja au mawazo yaliyotolewa na kundi la kwanza la wananafalsafa kuhusu lugha na mawasiliano.

Kundi hili la pili ndilo lilitoa msukumo mkubwa zaidi katika taaluma ya pragmatiki kama tunavyoijua na kuitambua leo.

Dai lao ni kuwa badala ya kung‘ang‘ania urasmi na usanifu wa lugha pamoja na ukweli na usikweli wake kama ndio msingi wa mawasiliano, tunapaswa kuchunguza namna ambavyo watu wa kawaida hufanikisha mawasiliano baina yao kwa kutumia lugha iyo hiyo inayodaiwa kuwa ni vurugu ili tuone wanawezaje kuwasiliana.

Katika kundi hili, wanafalsafa watatu wanatajwa kuwa ndio vinara na mashuhuri katika taaluma ya pragmatiki. Hao ni John L. Austin, John R. Searle na Herbert P. Grice.

JOHN L. AUSTIN

Mchango wake ni kuwa aliasisi nadharia ya tendo uneneni (1962)

JOHN R. SEARLE

Yeye aliboresha nadharia ya tendo uneni iliyoasisiwa na Austin. Uboreshaji huo ulifanyika (1969, 1975)

HERBERT P. GRICE NA KANUNI YAKE YA USHIRIKIANO

Huyu ni mwasisi wa kanuni ya ushirikiano katika mawasiliano (comparative principle) mwaka (1975).

Kanuni ya ushirikiano kwa mujibu wa Grice: Grice aliasisi kanuni ya mazungumzo iliyoitwa 'Logic in Conversation'. Kanuni hii inasema kuwa; toa mchango wako katika mazungumzo wakati wowote au unapozungumza kwa kuzingatia lengo kubalifu na mwelekeo wa mazungumzo unayojihusisha nayo.

Marejeo

1.      Massamba P. B. D (2004) Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.

2.      Mdee, J. S (1997), Nadharia na Historia ya Leksikografia, Dar es Salaam: TUKI.

3.      Morris, Charles W. (1971), Writings on the general theory of signs, The Hague: Mouton