http://www.swahilihub.com/image/view/-/4890032/medRes/2194553/-/xcsjbwz/-/maria.jpg

 

Sarufi miundo virai

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  13:26

Kwa Muhtasari

Muundo ni mpangilio wa vitu vidogo vilivyowekwa pamoja na kujenga kitu kikubwa zaidi.

 

SARUFI miundo virai ni mkabala wa kuchambua lugha kwa kuigawa sentensi katika virai vinayoiunda na kisha kuvichanganua zaidi hadi kufikia neno moja

moja lililokiunda kirai.

Tungo huundwa na viambajengo kwa utaratibu maalumu.

Tungo za lugha ni neno, kirai, kishazi na sentensi. Virai, vishazi na sentensi huundwa na

maneno.

 

MUUNDO WA KIRAI NA SENTENSI

Kirai, kishazi na sentensi ni vipashio vya lugha vinavyoundwa na viambajengo ambavyo ni vidogo kuliko vyenyewe.

Kirai hujengwa kwa maneno, na kishazi na sentensi hujengwa kwa virai. Viambajengo vya tungo ndivyo vinavyofanya muundo wa tungo husika.

 

MUUNDO WA KIRAI

Kirai ni fungu la maneno yanayohusiana kimuundo lisilokuwa na muundo wa kiima kiarifu. Maneno katika kirai humilikiwa na neno moja ambalo ndilo neno kuu. Kirai hubainishwa na kategoria ya neno kuu. Kwa mfano: KN, KT,KV, KE, KH na kadhalika.

Virai huundwa na viambajengo. Kiambajengo ni kikundi cha maneno au hata neno moja pia inayofanya kazi kama kitu kimoja. Kirai, kishazi au sentensi ni mkusanyiko wa viambajengo kadha. Kirai ni mkusanyiko wa viambajengo vilivyojengwa kuzunguka neno kuu.

Kwa mfano, KN huundwa na nomino na vivumishi vyake, kwa hivyo muundo wa kirai ni maneno yanayokiunda yakiwakilishwa na alama za kategoria za maneno hayo.

 

Kwa mfano:

‘Mtoto mdogo’.

Hiki ni Kirai Nomino (KN) kilichoundwa na N (nomino) na V (kivumishi).

 

Kwa hivyo KN = N+V 

‘analima shamba’.

Hiki ni kirai kitenzi (KT) chenye kuundwa na kitenzi (T) na kirai nomino

(KN). Kwa hivyo KT =T+KN

 

AINA ZA VIRAI NA SIFA KATIKA KISWAHILI

i. Kirai Nomino

ii. Kirai Tenzi

iii. Kirai Vumishi

iv. Kirai Elezi

v. Kirai Husishi

vi. Kirai Unganishi

 

MUUNDO WA VISHAZI NA SENTENSI

Kishazi ni kikundi cha maneno kilicho ndani ya sentensi chenye muundo wa kiima na kiarifu. Kishazi kina muundo sawa na sentensi.

Aina za vishazi na miundo yake

i. Vishazi ambatani

ii. Vishazi tegemezi