Sehemu ya Nne ya 'Usasa Usasambu'

Na WILLIAM HIMU

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  14:48

Kwa Muhtasari

Sehemu ya Nne ya 'Usasa Usasambu'

 

UTANGULIZI

Suala la utandawazi limekuwa ni jambo ambalo hatuwezi kuliepuka katika maisha yetu ya kila siku. Hata hivyo, suala hili limekuwa na matokeo hasi kwa watoto wetu wa kike na kusababisha kuwaathiri kimwili na kiakili. Kuingia kwa utandawazi kumewafanya vijana watumie muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii na intaneti ambako wanajifunza mambo mengi ya ovyo. Utandawazi una faida nyingi katika maendeleo ya binadamu kijamii, kisiasa na pia kiuchumi ila kwa nchi nyingi za ulimwengu wa tatu utandawazi umekuwa ni kaa la moto kwani kila anayejaribu kulishika lazima limuunguze. Kwa kuona hayo yote mwandishi wa tamthiliya hii ameamua kuifungua macho jamii ili iweze kuchukua hatamu kuwanusuru watoto hasa wa kike.

(Inaendelea kutoka Sehemu ya Tatu).

Mama Mwanaharusi: Soma, soma mwanangu! Achana na uchafu wa huo. Kumbuka wahenga walisema

dunia ni tambara bovu. Sasa wewe usiiendee kwa pupa. Tambua dunia haina siri, kwa sasa unaiona inayaficha unayodhani yako gizani, ipo siku itakuacha uchi.

Mwanaharusi: Mama, nisamehe sitorudia tena.

Mama Mwanaharusi: Kuwa na huruma kwa wazazi wako. Angalia tunavyohangaika kutafuta hela ili usome. Mama yako kutwa niko kwenye cherehani mpaka miguu inauma. Huna hata chembe ya huruma unacheza na shule?

Mwanaharusi: Naomba nisamehe mama, nisamehe mama yangu.

Mama Mwanaharusi: Baba yako anatoka usiku wa manane analala baharini usiku wote, baridi yake mvua yake, hatari ya papa na nyangumi  vyote vyake, yote hayo ni kwa ajili yako. Mtoto gani usiyekuwa na utambuzi?

Mwanaharusi: (Kimya huku akiwa anaangalia chini.)

Mama Mwanaharusi: Ona anavyoteseka na dhoruba za baharini, kwa nini huna huruma kwa wazazi wako? (Analia kwauchungu.) Nifanyaje ujue nakupenda mwanangu.

Mwanaharusi:Nimekuelewa mama, nakuahidi sitorudia tena mama yangu.

Mama Mwanaharusi: Sherehe mbili zilimshinda fisi na pia huwezi kupanda farasi wawili kwa mara moja, utapasuka msamba mwanangu.

Mwanaharusi:Nimekuelewa mama, nisamehe, nisamehe mama.

Mama Mwanaharusi: Naomba haya tuliyoongea yaishie hapa maana baba yako unamjua.

 

(Nyumbani kwa kina Mwanawima, anaingia baba Mwanawima  ametoka kwenye mihangaiko yake. Anafurahi kukuta mkewe na mwanaye wamekaa sebuleni wanaongea kwa utulivu.)

Baba Mwanawima: Hahaaa! Mama na mwana wamependeza! Yaani mmefanana kama pacha, hapo mke wangu umejizaa.

(Wote wanafurahi.)

Mama Mwanawima: Mwanao analalamika kichwa kinamuuma. (Baba Mwanawima anamsogelea mwanawe na kumgusa huku akimbembeleza.)

Baba Mwanawima: Pole, kunywa maji mengi utapata nafuu.

Mwanawima: Kila siku asubuhi kichwa lazima kiume, sijui kwa nini.

Mama Mwamawima: Au unasoma sana mwanangu.

Mwanawika: Mh! Hata sijui.

Baba Mwanawima:Unahitaji upate muda wa kupumzika kila siku walau saa nzima. Si kila muda ni kusoma tu.

Mama Mwanawima: Hakuna lolote, mvivu tu.

(Skuli ni muda wa mapumziko, majira ya saa nne asubuhi. Wanaonekana Mwanakombo, Mwanaharusi na Mwanawima wamekaa kwenye gogo la mnazi lililoanguka wanakula mihogo.)

Mwanaharusi: Jamani mimi kero za huyu mwalimu Bashiri zimenichosha.

Mwanakombo:  Kero gani? Wewe ni mtoto wa kike, hayo ni mambo ya kawaida sana... Kwani bado mnazungushana tu?

Mwanaharuusi: Tunazungushana? Mimi sina muda wa kuzungushana na mtu kama yule kwanza kidevu kimemchongoka kama kwato ya ng’ombe (Wote wanacheka.)

Mwanawima: Kwa nini usimkubalie, atakuharibia mambo yako.

Mwanaharusi: Hapana! Mama amenisema sana, ameongea mpaka akaanza kulia. Sitaki kumuudhi tena mama yangu.

Mwanakombo: Amelia? Yaani ile kesi ya simu tu ndio akuseme mpaka alie? Hapo labda kuna jambo jingine limejificha.

Mwanaharusi: Hapana sitaki kumuudhi tena mama, amenieleza uongo na uchafu wote wa wanaume.

Mwanakombo: Kweli kuna familia bado zimelala, yaani simu tu! Simu! Simu hii hii au?

Mwanaharusi: Jamani nimesema niacheni, sitaki kuwaudhi tena wazazi wangu. Inatosha!

Mwanawima: Basi kama hutaki wewe mdanganye tu uchukue hela zake.

Mwanaharusi: Hahaa, mla vya mwenzie na vyake huliwa, sina shida na hela kwa sasa.

Mwanakombo: Hata hufanani kuwa na sisi, unajifanya mstaarabu, eneee…

Mwanaharusi: Nyie ni rafiki zangu ila kwa hilo hapana, muonja asali haonji mara moja…

Mwanawima: Haya bwana, tuache sisi na yetu.

MWwanaharusi: Mimi kuna wazo nataka mnishauri, siwezi kuvumilia huu ujinga.

Mwanakombo: Wazo gani?

Mwanaharusi: Mimi nafikiria nikamsemehe kwa mkuu wa skuli. Najua ndio itakuwa mwanzo na mwisho wa kunisumbua.

Mwanakombo: Weee! Weeee! Weeee!      Nini? Tena usije ukafanya huo ujinga. Utajitafutia matatizo bure, wewe ni mwanamke, wanaume kukufuata ni lazima. Utatongozwa ukiwa kijana, ukiwa mama, ukiwa bibi, ukiwa mzuri au mbaya.  Mbona unajiwangia mtoto wa kike. Kaa ukijua bahati haiji mara mbili.

Mwanawima: Mwanamke muda wote wa maisha yake ni wa kusumbuliwa na wanaume. Kwa hiyo unavyotongozwa usijione wewe ndio mrembo sana hapa duniani.

Mwanakombo: Halooo, haloooo! Mwambie huyo, huu ndio muda wa kuutumia uzuri wako, ngoja mashavu yaanze kukuteremka uone kama utafuatwa.

Mwanawima: Sisi tunatongozwa na watu wengi kuliko hata wewe lakini ulishasikia tumemwambia nani? Acha ushamba wewe, jifunze kuweka mambo kifuani.

Mwanakombo: Ukiwaambia  wazazi wako kila mwanaume anayekutongoza si utamaliza kisiwa chote! Halafu utakuwa unajenga uhasama kwa watu. Umekuwa mtu mzima fanya uamuzi kwa busara.

Mwanawima: Huo ni utoto, tena wa chekechea.