http://www.swahilihub.com/image/view/-/4895246/medRes/2197893/-/1a5cdcz/-/wangari.jpg

 

Sentensi na miundo yake

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  16:55

Kwa Muhtasari

Sentensi ni kikundi cha maneno chenye maana iliyo kamili.

 

SENTENSI ndicho kipashio lugha cha kimuundo ambacho ni kikubwa kuliko vipashio vingine.

Vipashio vya lugha ni pamoja na: mofimu, neno, kirai, kishazi na sentensi yenyewe. Sentensi na kishazi huundwa na virai vikuu viwili: KN na KT. KT yaweza kuundwa na kitenzi na nomino, kitenzi na kielezi na kadhalika.

Kwa hivyo;

S=KN + KT

Sentensi na upatanishi wa kisarufi

 

SARUFI GEUZA UMBO ZALISHI

MAANA:

Nadharia ya Geuza Umbo Zalishi huonyesha ujuzi alionao mzungumzaji ambao humwezesha kutunga sentensi sahihi na zisizo na kikomo.

Uwezo wa mzungumzaji kutunga sentensi zisizo na ukomo unatokana na kufahamu kanuni za kutunga sentensi sahihi ambazo mzawa wa lugha anazijua kutokana na kuwa na umilisi na lugha yake.

Kanuni za kutunga sentensi sahihi hubainisha sentensi sahihi na zisizo sahihi.

Kwa mujibu wa nadharia hii, sentensi ina umbo la nje ambalo ndilo linalojitokeza katika usemaji na hata inapoandikwa, na umbo la ndani ambalo huwa limefichika na hujidhihirisha katika umbo jingine wakati wa kuongea (maana).

Nadharia hii imeweza kuonyesha uhusiano wa tungo ambazo japo zilikuwa na umbo la nje tofauti, zina umbo la ndani sawa.

 

Kwa mfano:

a) Nana anapika chakula.

b) Chakula kinapikwa na Nana.

 

Mfanano wa tungo hizi umekitwa katika maana. Ijapokuwa sentensi a) inaanza na Nana, na ile b) inaanza na chakula, mtenda na mtendwa katika sentensi zote ni yule yule.

Mchakato wa kubadili umbo la nje la sentensi a) na kuwa b) umesababisha uchopekaji wa kiunganishi ‘na’ na kiambishi tendwa ‘w’ katika kitenzi ‘pika’.

Kanuni geuzi tendwa ndiyo iliyotumika kuingiza mabadiliko haya.

Sentensi yaweza kubadilishwa kutoka umbo moja hadi jingine.

 

Kwa mfano:

a) Steve anafanya mtihani na Lulu anafanya mtihani.

b) Steve na Lulu wanafanya mtihani.

Umbo la nje la tungo hizi ni tofauti lakini umbo la ndani ni sawa. Tungo a) imedondosha baadhi ya maneno yaliyo katika b)

Kanuni ya udondoshaji imetumika kudondosha ‘anafanya mtihani’ ambayo imerudiwa katika sentensi a).

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo:

Richards, J.C., (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.

Wardhaugh, R., (1986). An Introduction to Socio- Linguistics. New York: Blackwell Publishers.

Ndungo, C. & Mwai, W. (1991). Kiswahili: Historical Modern Development in Kiswahili. Nairobi: University of Nairobi Press.

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com