Sifa bainifu za lugha (Sehemu ya Kwanza)

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Thursday, November 15  2018 at  07:02

Kwa Muhtasari

Lugha ina sifa bainifu ambazo ni; lugha ni mfumo, ni maalumu kwa binadamu, ni mfumo wa sauti nasibu, lugha ni mfumo wa ishara, lugha hutumia sauti na lugha ni kwa ajili ya mawasiliano.

 

LUGHA ni mfumo

Ishara zinazotumiwa katika lugha zina mpangilio wenye kutawaliwa na sheria na una ruwaza zinazotambulika na watumiaji wa lugha hiyo.

Kila lugha ya mwanadamu imeundwa katika mifumo miwili mikuu; mfumo wa sauti na mfumo wa maana.

Lugha huundwa kwa sauti ambazo huunganishwa kuunda neno au sehemu ya neno, maneno nayo huungana kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama virai, vishazi, sentensi na aya.

Katika muunganiko huu wa maneno na miundo mbali mbali, huwa kuna kanuni na sheria zinazidhibiti mfuatano wa kila kipashio.

Kuna kanuni zinazo dhibiti mfuatano wa sauti,mfuatano wa mofimu, mfuatano wa maneno na hata mfuatano wa sentensi.

Hivyo basi, mtu hawezi kuunganisha tu sentensi kwa matakwa yake bila kujali kanuni hizi, akifanya hivyo atasababisha kutokea kwa kitu ambacho siyo lugha na wala hakikubaliki katika lugha.

Kwa maana hiyo, lugha ya mwanadamu ni mfumo wenye kanuni, sheria na taratibu maalumu ambazo zikikiukwa basi kuna kuwa hakuna utimilifu wa lugha husika.

Lugha inaonyesha utaratibu katika mahusiano ya viunzi vya lugha. Sheria hizi zinazotawala mpangilio wa viunzi vya lugha hiyondizo zinazowawezesha watumiaji wa lugha fulani kuelewana

 

Lugha ni mfumo wa sauti nasibu (Unasibu katika lugha ya mwanadamu)

Lugha ni ya nasibu kwa maana kwamba, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno (mathalani kiti) na kitu chenyewe tunachotumia kukalia (maana na kirejelewa).

Hii ina maana kwamba, maumbo ya ishara za kiisimu hayana uhusiano wowote au mfanano wowote na maana ambazo tunayapa.

 

Lugha ni maalumu kwa mwanadamu.

Lugha ni chombo cha mawasiliano ambacho amejaaliwa binadamu tu na kwamba hakuna kiumbe mwingine ambaye si binadamu ana uwezo wa kuzungumza na kutumia lugha.

Hii ina maana kuwa kuna sifa fulani za lugha za binadamu ambazo hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote yule isipokuwa mwanadamu.

Ingawa ndege, mbwa, nyuki, tumbili wanawea kuwasiliana,mawasiliano yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo kimsingi siyo lugha, pia huwa yanadhibitiwana hisia tu kama hofu, njaa, na ishara za kutoa taarifa.

Binadamu ana uwezo wa kujifunza lugha mbalimbali na kutumia katika mazingira yake na sio wanyama.

Kwa mfano, ukimtoa mbwa Kenya na kumpeleka Ufaransa atatoa sauti ileile sawa na mbwa wa Ufaransa kwa kueleza shida ileile au kutoa ishara ileile.

Marejeo:

Chomsky Noam (1957) Syntactic Structures, The Hague, Mouton.

Tuki (1990) Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Paul, I. 1995 Vorgeschichtliche untersuchungen in Siebenburgen. Alba Iulia

Vlassa, N. 1965 --- (Atti UISPP, Roma 1965), 267–269