Sifa bainifu za lugha (Sehemu ya Pili)

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Thursday, November 15  2018 at  07:27

Kwa Muhtasari

Lugha ina sifa bainifu ambazo ni; lugha ni mfumo, ni maalumu kwa binadamu, ni mfumo wa sauti nasibu, lugha ni mfumo wa ishara, lugha hutumia sauti na lugha ni kwa ajili ya mawasiliano.

 

LUGHA ni mfumo wa ishara

Hii  inamaanisha kuwa maneno huambatanishwa au huhusishwa na vitu, matendo,mawazo au hisia kwa makubaliano ya unasibu tu.

Aidha, yale  tunayoyasoma katika maandishi ni ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika muktadha wa mawasiliano.

Hivyo basi,tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo wa alama za lugha hiyo na kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu vinavyowakilisha.

 

Lugha hutumia sauti

Sifa kuu ya lugha ni kutumia sauti ambazo hutengenezwa na ala za sauti. Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu ameyafikia kwa sasa katika uandishi na uwasilishaji wa taarifa kwa kutumia lugha sauti ndiyo msingi wa kila kitu.

Tafiti zinathibitisha kuwa mfumo wa maandishi umekuja baadaye sana katika maendeleo ya binadamu na kwamba hutumika tu kuwasilisha yale yanayosemwa kwa kutumia kinywa cha mzungumzaji.

Vile vile, ukweli kwamba binadamu anapozaliwa huanza kujua lugha ya mahala anapokua na kuishi kabla ya kufahamu kuandika,unatuthibitishia kiini cha lugha ni sauti.

Kwa ujumla, kuna sababu kuu tano zinazotuwezesha kukubaliana kuwa msingi wa lugha ni sautiza kutamkwa jinsi ifuatavyo:

  1. Mtoto hujifunza kuzungumza kabla hajajifunza kusoma na kuandika

  2. Mtoto hujifunza lugha moja kwam oja bila kufikiri kadiri anavyokuwa.

  3. Maandishi yalikuja baada ya mazungumzo

  4. Maandishi huwasilisha yale yanayozungumzwa

  5. Watu kwa kawaida hutumia muda mwingi kuzungumza kuliko kuandika

 

Kuna mambo mengi ya muhimu katika sauti za lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vyema kwa kutumia maandishi.

 

Mambo hayo ni kama vile kiimbo,toni, mkazo, kidatu ambayo ni muhimu katika mawasiliano lakini hayawezi kuwasilishwa kisawa sawa kwa kutumia maandishi (Habwe na Karanja, 2003).

 

Lugha ni kwa ajili ya mawasiliano

Kwa kutumia lugha binadamu anaweza kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi kuvifanya. Vile vile lugha hutuwezesha sisi kuzungumzia hisia zetu, matamanio yetu, kucheza,kufanya kazi na kadhalika.

Yote haya yanawezekana kwakuwa tunayo lugha ambayo ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano kwa jumla, lugha ni mfumo wa sauti nasibu zilizokubaliwa na watu au jamii ili zitumike katika mawasiliano yao ya kila siku kuelezea hisia, mawazo, mahitaji au matumaini yao.

 

marya.wangari@gmail.com

Falkenstein, A. 1965 Zu den Tafeln aus Tartaria. Germania 43, 269–273

Maxim, Z. 1997 Neo-eneoliticul din Transilvania. Bibliotheca Musei Napocensis 19. Cluj-Napoca

Paul, I. 1995 Vorgeschichtliche untersuchungen in Siebenburgen. Alba Iulia

Vlassa, N. 1965 --- (Atti UISPP, Roma 1965), 267–269