Sifa bainifu za lugha (Sehemu ya Tatu)

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Friday, November 16  2018 at  13:58

Kwa Muhtasari

Ishara katika lugha inamaanisha kuwa maneno huambatanishwa au huhusishwa na vitu, matendo, mawazo au hisia kwa makubaliano ya unasibu tu.

 

LUGHA ni mfumo wa ishara

Ishara katika lugha inamaanisha kuwa maneno huambatanishwa au huhusishwa na vitu, matendo, mawazo au hisia kwa makubaliano ya unasibu tu.

Aidha, yale tunayoyasoma katika maandishi ni ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika muktadha wa mawasiliano.

Hivyo basi,tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo wa alama za lugha hiyo na kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu vinavyowakilisha.

Lugha hutumia sauti

Sifa kuu ya lugha ni kutumia sauti ambazo hutengenezwa na ala za sauti.

Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu ameyafikia kwa sasa katika uandishi na uwasilishaji wa taarifa kwa kutumia lugha sauti ndiyo msingi wa kila kitu.

Isitoshe, tafiti zinathibitisha kuwa mfumo wa maandishi umekuja baadaye sana katika maendeleo ya binadamu na kwamba hutumika tu kuwasilisha yale yanayosemwa kwa kutumia kinywa cha mzungumzaji.

Vilevile, ukweli kwamba binadamu anapozaliwa huanza kujua lugha ya mahala anapokua na kuishi kabla ya kufahamu kuandika,unatuthibitishia kuwa msingi wa lugha ni sauti.

Kwa jumla, kuna sababu kuu tano zinazotuwezesha kukubaliana kuwa msingi wa lugha ni sautiza kutamkwa.

 

i.            Mtoto hujifunza kuzungumza kablra hajajifunza kusoma na kuandika.

ii.            Mtoto hujifunza lugha moja kwamoja bila kufikiri kadiri anavyokuwa.iii.

iii.            Maandishi yalikuja baada ya mazungumzo

iv.            Maandishi huwasilisha yale yanayozungumzwa

v.            Watu kwa kawaida hutumia muda mwingi kuzungumza kuliko kuandika

 

Kuna mambo mengi ya muhimu katika sauti za lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vyema kwa kutumia maandishi mathalan toni, mkazo, kiimbo, kidatu, ambayo  ni muhimu katika mawasiliano lakini hayawezi kuwasilishwa kisawa sawa kwa kutumia maandishi.

Lugha ni kwa ajili ya mawasiliano

Kwa kutumia lugha binadamu anaweza kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi kuvifanya.

Vilevile lugha hutuwezesha sisi kuzungumzia hisia zetu, matamanio yetu, kucheza, kufanya kazi Yote haya yanawezekana kwa kuwa tunayo lugha ambayo ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano.

Tabia za lugha ya binadamu ainazoitofautisha na aina nyingine za mawasiliano

Jinsi tulivyotaja awali, lugha ni maalumu kwa binadamu tu na kwamba hakuna kiumbe yeyote ambaye si mwanadamu mwenye uwezo wa kujua, kujifunza na kutumia lugha zaidi ya binadamu.

Jambo hili linatupelekea kuzitathmini sifa au tabia za lugha ya mwanadamu.Kimsingi sifa au tabia hizi ndizo zinazoitofautisha lugha ya mwanadamu na aina nyingine za mawasiliano zitumiwazo na wanyama.

 

 

Mareleo:

Chomsky Noam (1957) Syntactic Structures, The Hague, Mouton.

Tuki (1990) Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Paul, I. 1995 Vorgeschichtliche untersuchungen in Siebenburgen. Alba Iulia

Vlassa, N. 1965 --- (Atti UISPP, Roma 1965), 267–269