Sifa na uhusiano wa maana katika ngazi ya tungo

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Wednesday, September 27  2017 at  06:27

Kwa Mukhtasari

Katika makala iliyopita tulichambua na kuchanganua mada kuhusu sifa na uhusiano wa maana katika ngazi ya sentensi au tungo.

 

KATIKA makala iliyopita tulichambua na kuchanganua mada kuhusu sifa na uhusiano wa maana katika ngazi ya sentensi au tungo.

Tuliangazia vipengele kadha wa kadha na leo hii tutazidi kufahamishana jinsi ifuatavyo.

4. UPOTOO/ ANOMALI

Ni ukiushi wa kimantiki unaotokea pindi vijenzi-semantiki viwili siganifu vinapounganishwa kueleza jambo fulani. Kwa mfano:

a) Alichora barua kwa mguu wa kushoto (barua haichorwi-hata kama ingekuwa inachorwa basi haitachorwa kwa mguu bali kwa mkono, hivyo kuna upotoo)

b) Alimpiga teke kwa kalamu nyeusi (Hatupigi tege kwa kalamu bali kwa mguu)

c) Mjomba wangu ni mjamzito (mjomba hawezi kubeba mimba),

d) Rehema amemuoa Ramadhani (Mwanamke kwa utamaduni wa Kiswahili haoi bali anaolewa)

e) Aliandika barua kwa taa kubwa (tunaandika barua kwa kalamu wala sio kwa taa)

5. UZIADA-DUFU

Ni urudiaji usiohitajika au usio wa lazima au ni urudiaji usioongeza jambo jipya au taarifa mpya na wala hauufanyi ujumbe unaotolewa kuwa wazi zaidi. Kwa mfano:

Mke wangu ni mke wangu!*

Mwanafunzi ni mwanafunzi tu*

Rafiki yangu ni msichana wa kike

Msikiti ule wanaswalia Waislamu ( hakuna asiyejua kwamba msikitini wanaswali Waislamu)

NADHARIA ZA MAANA YA MAANA

Wataalamu mbalimbali wamebainisha nadharia mbalimbali za maana ya maana.

Zifuatazo ni baadhi ya nadharia hizo:-

1. Maana kama Kitajwa/Maana kama Kirejelewa

Nadharia hii hudai kuwa maana ya umbo la kiisimu ni kitu fulani halisi kinachotajwa na kurejelewa na umbo hilo.

Hivyo maana ya tamko ni kile kinachorejelewa na tamko hilo au kile ambacho neno husimama badala yake. Kama umbo lolote la kiisimu lina maana basi umbo hilo lazima liwe na kirejeleo chake. Kama maumbo mawili yanarejelea kitajwa kile kile au kitu kile kile basi maumbo hayo yana maana moja

2. Ubora wake

Ni kweli yapo maneno mengi katika lugha ambayo kazi yake ni kutaja vitu mbalimbali. Kwa mfano: nomino mahsusi, hata baadhi ya vitenzi halisi.

Nadharia hii ina ukweli kwa kiasi fulani kwa sababu watoto wanapojifunza lugha huanza na maumbo ya kiisimu ambayo yana vitu halisi vya kurejelea. Kwa mfano:

Mtoto ukimtuma kikombe anaweza akashindwa kujua lakini kama ukimwonyesha anaelewa zaidi.

3. Dosari/udhaifu

Katika lugha kuna maneno ambayo hayana virejelewa lakini yana maana.

Kwa mfano

neno 'na', 'hapana', 'kwa sababu', 'kwa', 'ya', na 'lakini'

Maneno haya yote yana maana katika lugha ya Kiswahili lakini hatuoni kitu chochote kinachorejelewa.

Tunaweza kuwa na matamko mawili tofauti yanayorejelea kitajwa kimoja lakini si lazima matamko hayo yawe na maana sawa kwani kuna uwezekano wa maumbo mawili sawa yakiwa na maana tofauti. Kwa mfano:-

Raisi wa Kenya

Kiongozi wa Jubilee

Amirijeshi Mkuu wa majeshi

Baba Ngina Kenyatta

Mumewe Margaret Kenyatta

Maumbo haya yote yanarejelea Rais Uhuru Kenyatta.

Kuna matumizi ya maneno ambayo hayarejelei kitu kinachotajwa.

Kuna maneno katika lugha ambayo hayarejelei kitu halisi.

Kwa mfano

neno 'kupe' kama neno la Kiswahili lina kirejelewa chake, yaani 'mdudu' lakini mtu anaweza kutumia neno 'kupe' akiwa na maana nyingine kabisa kwa mfano 'mnyonyaji'

Baadhi ya maneno hutaja vitu dhahania na hivyo kirejeleo chake hakipo

dhahiri. Kwa mfano: 'njaa', 'furaha', 'huzuni', 'kifo', 'uhai', na 'zimwi'

2. Maana kama Dhana

Nadharia hii inasema kwamba Maana ya umbo la kiisimu ni dhana au wazo linalohusishwa na umbo hilo.

Dhana ambayo imo akilini mwa mtu yeyote anayelijua umbo hilo la isimu. Kwa mujibu wa nadharia hii maneno ni alama ya mawazo yaliyo ndani ya akili ya mzungumzaji.