Sifa za kimsingi katika lugha

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Monday, November 19  2018 at  06:38

Kwa Muhtasari

Sauti za mwanadamu hupangwa kwa kufuata kanuni na taratibu za lugha ili kutupa maneno yenye maana.

 

Utamkaji pamwe (uwili)

LUGHA ya mwanadamu imepangwa katika viwango viwili ambavyo vinashirikiana na kukamilishana.

Kiwango cha kwanza ni kile kiwango cha utamkaji wa sauti au utoaji wa sauti kama; /n/, /m/, /g/, /t/, /k/, /a/, /e/, /o/ kwa kutumia alasauti mbalimbali.

Sauti hizi zikisimama peke yake hazina maana yoyote. Ni kama milio tu kama kupiga chafya, au makelele yanayotokana na kuburuza meza kwenye sakafu au kelele za injini ya pikipiki.

Sauti hizi zinapounganishwa - kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za lugha husika - tunapata maneno yenye maana ambapo tunapata kiwango kingine cha pili cha maana.

Sifa ya uwili inadhiririsha sifa ya uwekevu katika lugha ya mwanadamu kwani kwa kutumia sauti hizi chache mzungumza lugha anaweza kutoa au kuzungumza sentensi nyingi au tungo nyingi na zenye maana tofauti tofauti bila kikomo.

Suala jingine la msingi ni kwamba, tunaposema kuwa lugha imegawanyika katika viwango viwili, kiwango cha sauti na kiwango cha maana haimaanishi kwamba binadamu anatumia viwango hivi kiupeke peke.

Urejelezi au uhamisho

Uhamisho ni sifa ya lugha ya mwanadamu inayomaanisha kwamba lugha ya mwanadamu inaweza kutumika katika kuzungumzia au kurejelea kitu ambacho hakipo katika upeo wa macho ya mzungumzaji kiwakati na kimazingira. Tofauti na mawasiliano ya wanyama, binadamu anaweza kuzungumzia matukio yaliyopita, matukio yajayo, na hata yale anayoyatarajia kufanya kwa kutumia lugha. Kwa mfano, mnyama kama ng’ombe hawezi kuelezea kwa njia yake ya mawasiliano, aina ya chakula alichokula jana, au anachotamani kula, au anachotarajia kula, au kwa nini jana alikwenda kunywa maji, au hata kujua sababu ya kuumia.

Hata hivyo, mambo yaya haya binadamu anayaweza kuyaelezea kwa kutumia lugha yake ya asili au nyingine aliyojifunza.

Ubadilishanaji taarifa

Sifa hii inamaanisha kuwa binadamu wenyewe kama watumia lugha wana uwezo wa kubadilishana taarifa.

Kila mmoja wao anaweza kuwa mtumaji au mpokeaji wa taarifa kwa kutumia lugha.

Upekee

Sifa nyingine ni kwamba lugha huundwa na viunzi vidogo vilivyotengana na haipo katika mfululizo. Kila kipashio kinachotumika kuunda tungo za lugha kipo peke yake na kinaweza kuunganishwa na vingine kupata muundo wa juu mkubwa zaidi.

Hivyo basi, lugha inawezwa kugawanywa tena kwa kukusanya vipashio hivyo kuunda tungo kubwa zaidi.