Jazanda ya sumu katika tamthilia ya Kigogo

Na PHYLLIS MWACHILUMO

Imepakiwa - Thursday, April 12  2018 at  14:49

Kwa Muhtasari

Nyoka ni kiumbe anayeogopewa na wengi katika jamii kwa kuonekana kuwa ni muovu, mwenye hila na hatari.

 

KATIKA tamthilia ya Kigogo ya Pauline Keya, sumu ya nyoka imetumiwa na mwandishi ili kuwasilisha ujumbe wa kijazanda.

Kama tujuavyo, nyoka ni kiumbe anayeogopewa na wengi katika jamii kwa kuonekana kuwa ni muovu, mwenye hila na hatari. Anahushishwa na itikadi nyingi za kishirikina.

Sumu yake vilevile huwa kali hata zaidi. Katika tamthilia, nyoka aina ya swila ndiye anayetajwa na sumu yake kutumiwa.

Mojawapo ya jazanda ni pale ambapo watoto wa shule ya Majoka and Majoka Academy wanadaiwa kuwa mazuzu kwa kuwa wanadungana sumu ya nyoka. Sumu hii hapa huenda ikawa ni dawa za kulevya ambazo madhara yake huwa wazi kwa wanajamii wote.

Sumu pia huenda ikawa elimu yenyewe ambayo inaweza kuwa inaambatana na mafunzo yenye kuendeleza mambo yasiyokuwa na manufaa yoyote kwa wanafunzi hao au kwa jamii kwa jumla.

Mafunzo hayo huenda kuwa yanaendeleza kasumba za kuwapotosha watoto hao kiasi kuwa mwandishi ameonelea ni bora kuwasawiri kama mazuzu! Uzuzu wao huo ukawa unasababishwa na sumu hiyo ya swila.

Hata hivyo, mwandishi anaonyesha kuwa athari za sumu haziwasazi wale wenye uhusiano wa karibu na mmiliki wa nyoka mwenyewe. Hivyo basi, mwanawe kiongozi yaani mwana wa Mzee Majoka mwenyewe pia anaumwa na nyoka wa babake na kufariki.

Hivi ni kusema kuwa maovu wanayowapangia wananchi hata viongozi wenyewe huathirika nayo. Ukimchimbia mwenzio kisima, kumbe utatumbukiawewe mwenyewe!

Hapo kulikuwa na onyo kwa viongozi wenye kuendeleza maovu wakidhani kuwa yatawaumiza wengine tu ila si wao wenyewe.

Sumu ya nyoka pia ilitumia kama njia ya kuwatisha raia na hata kuwaadhibu iwapo hawangetekelea waliyohitajika.

Ngurumo aliuwawa kwa kutumia sumu hii ya nyoka.
Kama ilivyokuwa katika tamthilia, kiongozi majoka alikuwa na kiwanda kikubwa cha kuitengeneza sumu hii.

Bila shaka ni maajabu kuona kuwa kiongozi anajifaidisha kwa bidhaa yenye kuleta uharibiru katika jamii ilhali yeye anafurahii faida yake!

Mwandishi bila shaka anatumia sumu hii kijazanda ili kumfumbia msomaji fumbo hilo.