Ubora na udhaifu wa Sarufi Zalishi katika Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Wednesday, October 31  2018 at  06:51

Kwa Muhtasari

Nadharia ya Sarufi Zalishi ina ubora na udhaifu wake.

 

TUMEKUWA tukichambua na kutathmini kwa kina mada kuhusu nadharia ya sarufi zalishi katika lugha ya Kiswahili.

Kama tu nadharia nyinginezo, nadharia ya Sarufi Zalishi ina ubora na udhaifu wake jinsi ifuatavyo:

 

Ubora wa nadharia ya Sarufi Zalishi

  1. Imeweza kuonyesha umilisi alionao binadamu katika lugha yake, kuwa anaweza kuzalisha tungo au sentensi mbalimbali kwa kutumia kanuni chache zilizopo katika lugha yake. Umilisi huo humsaidia mtumiaji wa lugha kuunda sentensi hizo hata kama hajui kusoma na kuandika.

  2. Nadharia ya sarufi zalishi inaonyesha kuwa kila mzungumzaji wa lugha huzifahamu vizuri kanuni chache zilizopo katika lugha yake na kuzitumia kanuni hizi katika kuwasiliana na jamii inayomzunguka.

  3. Nadharia hii imeweza kuonyesha kuwa binadamu anao uwezo wa kufafanua kipi ni sahihi na kipi sio sahihi katika uteuzi wa maneno wakati wa uzungumzaji.

  4. Nadharia hii inamchukulia binadamu kama kiumbe chenye uwezo endelevu wa kuzalisha sentensi ambayo inaweza kueleweka kwa jamii inayomzunguka.
  5. Nadharia ya sarufi zalishi inatuonyesha kwamba upo uhusiano mkubwa kati ya akili, kufikiri na lugha. Hususan katika dhana ya utendaji mtumiaji wa lugha anatakiwa kutumia akili anapoteua lugha ya kutumia ili kuendana na muktadha husika.

 

Udhaifu wa nadharia ya Sarufi Zalishi

  1. Inafafanua namna au jinsi watu wanavyozungumza lugha na sio kuwaeleza wazwanavyopaswa kuzungumza lugha hiyo.

  2. Haitilii mkazo mabadiliko katika lugha hata kama yapo.

  3. Vipengele kama umbo la ndani na umbo la nje vinaweza kumchanganya mtu anaejifunza lugha.

 

Ni bayana kuwa nadharia ya Sarufi Zalishi imeleta mapinduzi makubwa katika taaluma ya sarufi miundo au ukipenda sintaksia.

 

Sintaksia ya Kiswahili (sarufi miundo/muundo)

Ni tawi la isimu au taaluma ya sarufi inayoshughulikia namna ambavyo vikundi vya maneno na sentensi.

mbalimbali zinajengwa katika lugha.

Kwa mukhtasari, sintaksia hushughulikia kanuni zinazotawala mfumo wa vipashio vya lugha. Aidha,

Sarufi muundo hushughulikia kanuni zinazotawala mpangilio wa maneno katika lugha husika ili kujenga

(kuunda tungo yenye maana).

 

Kipashio ni kipande cha neno au kikundi cha maneno yanayotoa taarifa fulani katika lugha ya Kiswahili.

Kuna vipashio vitano jinsi ifuatavyo:

Mofimu – Neno – Kirai- Kishazi - Sentensi.

 

Wasiliana na mwandishi kupitia baruapepe: marya.wangari@gmail.com