Ubora wa nadharia za chimbuko la Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Thursday, November 22  2018 at  12:31

Kwa Muhtasari

Lugha ya Kiswahili ilizungumzwa mara ya kwanza eneo la pwani ya Afrika Mashariki.

 

Kutoka kwa: Martha Magomela

Swali: Nitajie ubora wa nadharia za chimbuko la Kiswahili

 

KATIKA makala ya leo, tutaangazia na kuchambua kwa kina mada kuhusu nadharia za chimbuko la lugha ya Kiswahili katika juhudu za kujibu swali lililoulizwa na msomaji wetu.

Lugha ya Kiswahili inazungumzwa na zaidi ya watu milioni mia moja kote ulimwenguni. Ni  lugha ya saba ulimwenguni na ya pili barani Afrika kwa kuwa na wazungumzaji wengi. Isitoshe, ni lugha ya kitaifa na lugha rasmi nchini Kenya na Tanzania.

Aidha, ni moja kati ya lugha rasmi katika vikao vya Umoja wa Afrika. Lugha ya Kiswahili ilizungumzwa mara ya kwanza eneo la pwani ya Afrika Mashariki.

Historia ya Kiswahili imegawanyika katika vipindi tofauti katika ukuaji na ueneaji wake.

Hata hivyo, chimbuko la lugha ya Kiswahili limefafanuliwa na wataalam wengi kupitia hoja mbalimbali.

Ni kwa mintarafu hii ambapo suala la asili ya lugha limesalia kuwa mjadala mrefu.

Asili ya lugha ya Kiswahili imetafitiwa na wanaisimu na wanahistoria na wamezuka na nadharia zinazokinzana.

NADHARIA KUHUSU CHIMBUKO LA KISWAHILI

Neno chimbuko lina maana ya mwanzo au asili ya kitu.

Wanaisimu kadha wamejaribu kuchunguza asili ya lugha ya Kiswahili na kuibua nadharia anuwai jinsi ifuatavyo:

Nadharia kuwa Kiswahili ni lahaja ya Kiarabu

Baadhi ya wataalamu wanashikilia mtazamo kuwa Kiswahili ni mojawapo ya lahaja za Kiarabu kwa sababu ya kuwepo na idadi kubwa ya msamiati wa Kiarabu katika Kiswahili.

Wanadai kuwa asili ya jina Kiswahili limetokana na neno la Kiarabu sahil kwa maana ya pwani. Wingi wake ukiwa sawaahil.

Vilevile, wanadai kwamba idadi kubwa ya wenyeji wa pwani ni Waislamu dini iliyoletwa na Waarabu.

Wanafafanua kwamba, ikiwa Kiswahili kilianza pwani na wasemaji wake ni Waislamu, basi hata nacho kilitoka Uarabuni.

Aidha, wanaoshikilia nadharia hii wanasema kuwa Kiswahili ni tokeo la ndoa baina ya wanawake wa pwani ya Afrika Mashariki na Waarabu; kwamba watoto waliozaliwa walizungumza Kiarabu.

Udhaifu wake

Udhaifu wa nadharia hii unajitokeza kwa namna hii: Inawezekana vipi, kwa mfano, mtu mwenye asili ya Kikuyu na Mluo kuoana na kisha mtoto wao aongee lugha ngeni.

Na je, kwa nini lugha ya Kiingereza ambayo ina asilimia takribani 70 ya maneno ya Kilatini na Kiyunani (Kigiriki cha kale) haiitwi lugha ya vizalia?

 

Marejeo

Mehrabian na Ferris (1967). "Inference of Attitude from Nonverbal Communication in Two Channels". Katika: The Journal of Counselling Psychology Vol.31, 1967, pp.248-52.

Witzany, G. (2006 Plant Communication from Biosemiotic Perspective. Plant Signaling na Behavior 1 (4): 169-178.