http://www.swahilihub.com/image/view/-/4890032/medRes/2194553/-/xcsjbwz/-/maria.jpg

 

Ufafanuzi wa dhana ya Nadharia kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  12:20

Kwa Muhtasari

Kwa mujibu wa Sengo (2009), nadharia imefasiriwa kama wazo kuu, fikra kuu, mwongozo mkuu wa mtu, watu au jamii ya pahala fulani, wakati fulani na kwa sababu fulani.

 

TUKIREJELEA mawazo ya Sengo, tunaweza kufasiri dhana hii kuwa dira na mwongozo wa kulikabili jambo kifalsafa, kidini, kimantiki, kijamii na kiutamaduni. Vilevile, nadharia inaweza kuelezwa kuwa ni mawazo au mwongozo unaomwongoza mtafiti au mchambuzi wa jambo fulani ili kuweza kulikabili jambo hilo ambalo halijapata kupatiwa uvumbuzi au ukweli wake.

TUKI (2004) nao wanafasiri nadharia kuwa ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kutekeleza jambo fulani. Kwa upande wake Wafula R. M(2004) nadharia husheheni mwongozo wa mikakati ya usomaji wa kazi ya fasihi na hucheza nafasi ya dira katika kuhakiki na kufanya uamuzi fulani.

Nao wasomi Wafula na Njogu (2007), wanafafanua na kupambanua nadharia kuwa jumla ya maelekezo yanayomsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu.

Wanadokeza zaidi kuwa dhana hii hurejelea istilahi ya kijumla inayomaanisha mwongozo unaomwelekeza msomaji wa kazi ya fasihi kuifahamu kazi hiyo vizuri katika vipengele mbalimbali vya kazi ya fasihi na namna vinaunganika kuleta umoja katika kazi husika.

Kwa mfano jinsi maudhui hulingana na mandhari au jinsi mandhari yanavyolingana na wahusika katika kazi ya fasihi.

Kauli za kijumla

Kulingana na Mwalimu Wamitila (2003), nadharia hutumiwa kumaanisha kauli za kijumla au kaida zinazomwongoza msomaji katika ufasiri wa maana uliopo katika fasihi.

Kwa mfano katika kuelewa maudhui katika kazi ile ya fasihi.

Fauka ya hayo, anasema kuwa ni njia ya kisayanzi inayohusika na kanuni za kijumla na zinazohusika katika utatuzi wa swala fulani katika kazi ya kifasihi na pia ni nyenzo ya kufikia malengo fulani ya kiusomi. 

Hata hivyo, nadharia za kuhakiki ni nyenzo tu ya kutusaidia kulifikia lengo fulani ambapo kila nyenzo huwa na ubora na udhaifu.

Aidha,nadharia huzuka katika mazingira maalum ambayo yana wasifu na utamaduni mahususi.

Hivyo basi, hatupaswi kupofushwa na nadharia kiasi cha kutotambua kuwa zina udhaifu wa kuvimulika vipengele fulani vinavyohusiana na lugha na fasihi zetu.

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo:

Achebe, C. (1988). Hopes and Impediments. London: Heinemann.

Kezilahabi, E. (1974). Kichomi. Nairobi: Heinemann.

Wamitila, K. W. (2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus.

Wa Thiong'o, Ngugi (1998). Penpoints Gunpoints and Dreams. Oxford: Clarendon.