http://www.swahilihub.com/image/view/-/4890032/medRes/2194553/-/xcsjbwz/-/maria.jpg

 

Historia ya ukuaji na maendeleo ya uundaji wa istilahi za Kiswahili

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  13:27

Kwa Muhtasari

Mpaka kati ya istilahi na msamiati ni finyu.

 

ZUBEIDA (1995), anasisitiza kwamba, mpaka kati ya istilahi na msamiati ni finyu hasa pale ambapo maneno ambayo asili yake ni msamiati wa jumla hutumika kama istilahi katika Nordic Journal of African Studies 338 uwanja maalumu.

Kazi ya kuyapatia maneno ya kawaida hadhi ya istilahi huhitaji uelewa mkubwa wa maneno ya lugha na maana zake kama zilivyofasiliwa katika kamusi za kawaida.

Ubainishaji wa tofauti kati ya teminografia na leksikografia ya lugha ya kitaalamu, unatujengea msingi wa kuweza kupima na kuamua kama uundaji wa istilahi za Kiswahili umekuwa ukizingatia teminografia au leksikografia ya lugha ya kitaalamu.

MCHAKATO WA UUNDAJI WA ISTILAHI ZA KISWAHILI

Mwanasoko (1992) anajadili kuwa, pamoja na kwamba kazi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili umekuwa ukiendelea tokea mwaka 1930, ongezeko la ghafla la mahitaji ya istilahi za Kiswahili lilijidhihirisha baada ya mwaka 1967 pale Kiswahili kilipotangazwa kuwa lugha rasmi ya kuendeshea shughuli za serikali pamoja na kufundishia elimu ya msingi.

Katika kukabiliana na hali hiyo, mwaka 1967 Serikali iliunda Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambalo, pamoja na majukumu mengine, lilikabidhiwa jukumu la kusimamia na kuratibu uundaji wa istilahi sanifu za Kiswahili kwa ajili ya matumizi ya Kiswahili, hususani katika ofisi na idara za Serikali.

Katika miaka ya 1970, ongezeko la mahitaji ya istilahi, hasa kwa ajili ya matumizi katika elimu, lilichochea asasi kadhaa za kitaaluma kujiingiza katika utafiti na ukuzaji wa istilahi za Kiswahili.

Asasi hizo ni pamoja na iliyokuwa Taasisi ya Ukuzaji Mitaala ambayo baadaye ilibadilika kuwa Taasisi ya Elimu Tanzania, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) na Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Hata hivyo, miongoni mwa asasi hizi, TUKI imejitokeza zaidi katika suala zima la ukuzaji wa istilahi za Kiswahili.

Kwa hali hiyo, katika sehemu mjadala wetu tutatumia mifano ya istilahi za BAKITA na za TUKI katika kubainisha mwelekeo wa mkabala na mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili.

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo:

Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.

Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi Kenya: Longhorn Publishers.

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com