http://www.swahilihub.com/image/view/-/3392154/medRes/1442811/-/wo81ep/-/Harare.jpg

 

Ukuzaji na uendelezaji wa Kiswahili nchini Zimbabwe

Harare

Jiji kuu la Zimbabwe, Harare. Picha/MAKTABA 

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Friday, September 23  2016 at  10:28

Kwa Mukhtasari

Juhudi mbalimbali zinafanywa na mabingwa wa Kiswahili kutoka Tanzania za kufundisha lugha ya Kiswahili katika ngazi mbalimbali nchini Zimbabwe.

 

JUHUDI mbalimbali zinafanywa na mabingwa wa Kiswahili kutoka Tanzania za kufundisha lugha ya Kiswahili katika ngazi mbalimbali nchini Zimbabwe.

Hii ni hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Zimbabwe ya kutaka Kiswahili kifundishwe katika shule za msingi na sekondari.

Ili kutekeleza azma hii walimu wawili wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (TATAKI) waliteuliwa kuenda Zimbabwe kwa shughuli za kufundisha Kiswahili nchini humo.

Hatuna budi kuwapongeza viongozi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili kwa kukubali ombi hili la kuanzisha mawasiliano na Chuo Kikuu cha Harare nchini Zimbabwe.

Mpango wa kupeleka walimu wa kufundisha Kiswahili nchini Zimbabwe ulihitaji maandalizi kwa pande zote mbili zinazohusika.

Kwanza nchini Zimbabwe zilihitajika juhudi za kisera za kukubali Kiswahili kifundishwe katika shule za msingi na sekondari. Pili, kwa upande wa Tanzania walimu wa TATAKI walitakiwa kujiandaa kutayarisha mtalaa wa kufundisha somo la Kiswahili.

Mtalaa huu unafuatiwa na utayarishaji wa vitabu, vielelezo na matini ya kufundishia na kujifunzia.

Ilishauriwa kuwa kwa kuanzia, somo hilo lianze kufundishwa katika Chuo Kikuu cha Harare kwa lengo la kuwapata walimu na wataalamu ambao watasaidia kufundisha Kiswahili kuanzia shule za msingi na sekondari.

Hivyo, darasa la wanafunzi 80 lilianzishwa mwaka 2012 na kusimamiwa na walimu wenye uzoefu katika taaluma ya Kiswahili.

Miongoni mwa walimu hao ni Titus Mpemba ambaye amewahi kufundisha darasa maalumu kwa wahariri, wahakiki na waandishi wa Kiswahili wa gazeti la Mwananchi na Mwanaspoti katika Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), lililolenga kuwanoa wafanyakazi walio katika Idara ya Uhariri ili wawe mahiri zaidi katika matumizi ya Kiswahili yaliyo fasaha na sanifu katika kazi yao ya uandishi wa habari.

Ari ya kujifunza zaidi

Hata hivyo, licha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia kwenye ngazi ya shule za msingi na sekondari, bado wanafunzi na wananchi wa kawaida wa Zimbabwe wangependa kujifunza zaidi lugha hii.

Njia mojawapo ni kwa kutumia mitandao ya kijamii kama Facebook, Twitter na Whatsap. Pamoja na mitandao hii, iko tovuti ijulikanayo kama Swahili Hub (www.swahilihub.com) chini ya usimamizi wa Kampuni ya Nation Media Group.

Tovuti hii ina uwezo wa kusambaza masuala mbalimbali ya lugha ya Kiswahili kama fasihi na isimu ya lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi wa wanaoanza kujifunza Kiswahili, (Ngazi ya awali) na pia wanaotaka kujiendeleza zaidi (Ngazi ya kati).

Nalo gazeti la Mwananchi lina fursa kubwa ya kukieneza Kiswahili kwani wanafunzi wanaotaka kujifunza Kiswahili kwa njia zilizo rasmi (shuleni) na wale walio katika mfumo usio rasmi (nje ya darasa) wataweza kunufaika kwa kutumia ama Tovuti ya Swahili Hub au kwa kutumia mtandao wa e-paper.

Zaidi ya hayo, mtandao wa Swahili Hub unafanya mpango wa kutayarisha benki ya majina ya vituo, vyuo shule na pia watafiti na wahadhiri wa Kiswahili duniani kote kwa lengo la kukusanya kazi zao za uhariri na uchapishaji wa makala, vitini na vitabu vya Kiswahili.

Benki hii itatumika kama chanzo cha taarifa kuhusu masuala mbalimbali ya Kiswahili kwa ajili ya marejeleo.

Wazungumzaji wa Kiswahili nchini Zimbabwe wanaweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwamo kukuza uelewa wa matumizi sanifu ya lugha ya Kiswahili kupitia makala za kitaaluma zinazopatikana katika mtandao huu wa Swahili Hub.

Mpango huu wa kufundisha Kiswahili nchini Zimbabwe unatakiwa kuelekezwa pia katika baadhi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Uganda, Sudan Kusini, Burundi na Rwanda.

Lengo ni kuraghbisha maendeleo ya mawasiliano katika nyanja za uchumi, siasa, elimu, utamaduni na masuala mengine ya kijamii. Itawekana kama Kamisheni ya Kiswahili iliyo chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye makao yake huko Zanzibar itatekeleza wajibu wake barabara.

Nazo serikali za jumuiya hii ziwe na utashi wa kisiasa na kuweka uzalendo mbele kwa kutoa fedha za kutosha kuendeshha mpango huu.

Mawaziri wa Utamaduni wa nchi za Afrika wakumbuke kuwa mwaka 1988 walikutana Mauritius na kuridhia kukifanya Kiswahili kuwa ni lugha ya kazi katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika (wakati huo OAU) badala ya lugha kubwa kama Kiigbo, Kihausa na Kiwolof huko Afrika Magharibi.

Pia wakumbuke kuwa wakati wa ukoloni Kiswahili kilikuwa kikikuzwa kwa kusanifiwa chini ya uongozi wa Kamati ya Lugha (Kiswahili) ya Afrika Mashariki kuanzia mwaka 1930.

Je, viongozi wa sasa wanasubiri nini kukiendeleza Kiswahili ili kitamalaki katika maisha ya wanajumuiya wote? Swali hili litajibiwa na wanaoshika hatamu katika serikali zetu.

Stephenjmaina1965@yahoo.com

Smaina1@tz.nationmedia.com