Usasa Usasambu

Na WILLIAM HIMU

Imepakiwa - Tuesday, June 5  2018 at  13:55

Kwa Muhtasari

  • Maudhui ya Usasa Usasambu yanagusia maeneo ambayo vijana wengi wanataka kujikita kama sehemu ya burudani
  • Soma ili ufahamu mengi kuhusu vijana hasa wa kike wanavyoathirika na utandawazi

 

UTANGULIZI

HIKI ni kitabu kilichopedekezwa kusomwa katika shule za msingi na madarasa ya chini ya shule za sekondari kidato cha kwanza na cha pili.

Maudhui yake yanagusia maeneo ambayo vijana wengi wanataka kujikita kama sehemu ya burudani. Soma hadithi hii ili ufahamu mengi kuhusu vijana hasa wa kike wanavyoathirika na utandawazi.

 

Suala la utandawazi limekuwa ni jambo ambalo hatuwezi kuliepuka katika maisha yetu ya kila siku. Hata hivyo, suala hili limekuwa na matokeo hasi kwa watoto wetu wa kike na kusababisha kuwaathiri kimwili na kiakili. Kuingia kwa utandawazi kumewafanya vijana watumie muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii na intaneti ambako wanajifunza mambo mengi ya ovyo. Utandawazi una faida nyingi katika maendeleo ya binadamu kijamii, kisiasa na pia kiuchumi ila kwa nchi nyingi za ulimwengu wa tatu utandawazi umekuwa ni kaa la moto kwani kila anayejaribu kulishika lazima limuunguze. Kwa kuona hayo yote mwandishi wa tamthiliya hii ameamua kuifungua macho jamii ili iweze kuchukua hatamu kuwanusuru watoto hasa wa kike.

 

Onesho la Kwanza

(Hali ya hewa ni ya baridi kiasi.  Upepo unavuma kwa kasi na kuifanya bahari ichafuke. Miti inayumba kulia na kushoto kufuata upepo. Minazi nayo imetapakaa kila kona ya skuli, inacheza sawa na mvumo wa upepo. Wanafunzi wanakimbizana huku na huko kila mmoja akiwa anawahi kurudi nyumbani. Kando ya barabara nje kidogo ya maeneo ya shule, wanaonekana Mwanakombo, Mwanawima na Mwanaharusi wanaelekea kwenye kituo cha dala dala kurudi nyumbani kwao.)

Konda: (Konda anawazuia mlangoni) Wanafunzi mwisho watatu, wakusoma mnatoshaaa! Mnatoshaa hamsikii? Hili sio gari la watoto wa Serikali bwana!

Mwanawima: Heee, wee koma! Usinishike na mi – mikono yako. Hujui pesa ya sabuni inapotoka, hebu pisha huko! (Anatumia nguvu kuingia.)

Konda: Kaa mbali, watu wako kazini, tusileteane uzuri hapa…

Mwanakombo: Heee heee, halooooo, hiyo nayo kazi? Muda wote unanuka vikwapa. (Abiria wanageuka na kumuangalia Mwanakombo.)

Konda: (Anamkata jicho na kushindwa kujizuia, anamjibu) Kwako kazi nzuri ni zipi? Au ni zile za baba zenu kushinda majini kama vyura? (Abiria wote  wanacheka.)

Mwanawima: Kwenda mwana kwenda, uvuvi ndio shughuli kuu ya uchumi hapa kisiwani wewe ulitaka awe anachungulia kwenye mlango wa daladala kama wewe?

Konda: Akalime karafuu anukie ili atoe shombo la samaki. Si wataka visivyonuka?

Mwanaharusi: (Anawanyamazisha wenzake) Hebu acheni kupayuka. Tumechoka na kelele tulikotoka. Tupumzisheni jamani.

Dereva:(Anageuka nyuma) Oyaa usigombane na wa kusoma. Hao ndio matajiri wetu wa kesho. Angalia vichwa mwanangu siku mbaya hii.

Konda:(Gari linaenda huku konda anaendelea kuita abiria) Haya Stonetown kwa wajanja twendee…

 

(Itaendelea sehemu ya pili)