Usasa Usasambu

Na WILLIAM HIMU

Imepakiwa - Wednesday, July 18  2018 at  06:44

Kwa Muhtasari

Usasa Usasambu; teknolojia inaharibu mambo kwa kiasi fulani.

 

Sehemu ya Saba A

 

Mwanakombo: Mimi nakuhakikishia kuwa Mwanaharusi anakupenda, kukaa kimya haimaanishi kuwa hakutaki bali anataka aone msimamo wako.

Dulla: Acha uongo, kuna tetesi nimezipata kuwa anatembea na mwalimu Bashiri ina maana wewe huzijui?

Mwanakombo: Ukimchunguza sana bata hutomla, huo ni uvumi tu.

Dulla:Na mnavyojua kufichiana siri, wallah nikijua nawaharibia, bora tukose wote.

Mwanakombo:Hakuna lolote, mwalimu hawezi kumpata, yule ni wako.

Wewe kaza kamba tu.

Dulla: Tatizo lenu wanawake mkijijua ni wazuri mnaringa sana!

Mwanakombo:Hahaaa! Lazima turinge, hivyo ndio tulivyoumbwa.

Dulla: Muite basi niongee naye…

Mwanakombo:(Anaita) Mwanaharusi njoo mara moja (Mwanaharusi

anaenda kwa madaha)

Mwanaharuusi: Enheee, niambie unasemaje! (Amekunja mikono yake kifuani)

Dulla: Nimekuita tuongee kidogo, mbona unauliza kwa ukali hivyo?

Mwanakombo:Jamani naenda uani mara moja (Anawaacha

Mwanaharusi na Dulla.)

Dulla: Vipi mbona unanizungusha sana! (Kwa sauti ya chini.)

Mwanaharusi:Nakuzungusha na nini?

Dulla: Nakupenda sana Mwanaharusi, kwa nini hautaki kunielewa?

Mwanaharusi: Ndio mlivyodanganyana na huyo mwenzako sio? Sasa naomba kuanzia leo ukome kunifuatilia, koma kabisa.

Dulla: (Anavuta pumzi kwa nguvu) Hapana nisikilize kwanza.

Mwanaharusi: Nimemaliza (Anamsonya kisha anaondoka.)

Dulla: Subiri Mwanaharusi, subiri kwanza nina zawadi yako…

Mwanaharusi: Nikuulize swali?

Dulla:Sawa niulize tu nakusikiliza (Huku akiendelea kutoa zawadi yake kwenye mfuko.)

Mwanaharusi: Mimi na mama yako unampenda nani?

Dulla:Sasa hayo maswali gani tena hapa?

Mwanaharusi:Nijibu tu.

Dulla:Nampenda mama.

Mwanaharusi:(Anashika kiuno) Una miaka mingapi haujampa mama yako zawadi.

Dulla:(Kimya) Aah hayo ya mama yaache kwanza.

Mwanaharusi: Basi naomba hiyo zawadi nenda kampe mama yako, mimi sina shida na hiyo zawadi. (Anaondoka kwa dharau.)

Dulla:(Anasikitika kwa kutingisha kichwa huku akiongea kimoyo moyo) Hizo dharau zitaisha tu labda usiingie kwenye himaya yangu.

(Kelele za cherehani zinaendelea kusikika nyumbani kwa mama Mwanaharusi. Muda wote mama Mwanaharusi anajishughulisha kuhakikisha anasaidiana na mumewe kuendesha familia. Punde kidogo anaingia Mwanaharusi.)

Mwanaharusi:Shikamoo mama.

Mama Mwanaharuusi:Marahabaa, habari za skuli? (Anaacha kushona na kumsikiliza mwanae.)

Mwanaharusi: Nzuri tu (Kimya kidogo huku anamwangalia mama yake.)

Mama Mwanaharusi:Vipi kuna tatizo lolote?

Mwanaharusi:Hapana mama, pole kwa kazi. Nakuonea huruma unavyohangaika kwa ajili yangu mama.

Mama Mwanaharuusi:Mmmh! Asante sana mwanangu, usijali ndio maisha, pita ndani kaangalie chakula (Anaendelea kushona. Mwanaharusi anaingia ndani huku akiendelea kumwangalia mama yake anavyoshona, anaenda kuchukua chakula na kurudi kuendelea kukaa na mama yake.)

Mwanaharusi:Mama! Mitihani inakaribia hivyo nahitaji muda zaidi wa kujiandaa.

Mama Mwanaharusi:Usijali, wewe jiandae tu mwanangu, hamna kazi ya kunishinda humu ndani.

MWANAHARUSI: Mmmh! Si utachoka sana mama.

Mama Mwanaharusi: Hapana, nataka na wewe ufikie malengo yako, sisi wazazi wako tulikosa elimu na wewe ukikosa itakuwaje?

Mwanaharusi: Sawa, nashukuru mama ila… (Anasita kidogo.)

Mama Mwanaharusi: Ila nini…?

Mwanahabari: Aaaah, basi nitakuambia siku nyingine. (Alitaka kumueleza usumbufu wa mwalimu Bashiri.)

Mama Mwanahabari: Sema tu, mtoto wa kike siri zake zote ni kwa mama yake. Yote unayoyapitia mimi niliyapitia.

Mwanahabari:Ni kweli mama, nashukuru kwa kuniongoza mpaka hapa nilipofika.