Usasa Usasambu

Na WILLIAM HIMU

Imepakiwa - Wednesday, July 18  2018 at  06:50

Kwa Muhtasari

Usasa Usasambu; teknolojia inaharibu mambo kwa kiasi fulani.

 

Sehemu ya Saba B

 

Mwl. Bashiri:(Anaichukua na kuisoma taratibu, anahamaki) Heeeee! Hii ni nini?

Mwanaharusi: Samahani mwalimu, nilikuwa nafikiria hatima yako ni nini baada ya kukukubalia, nafsi ilinisuta ndio maana nimeamua nikuweke wazi ili ujue.

Mwl. Bashiri:Siamini, umeathirika, una virusi vya Ukimwi?

Mwanaharusi:Ndio! (Analia huku mikono ikiwa imefumba macho  yake) Mimi nimezaliwa nikiwa na virusi vya Ukimwi. Inaniuma natamani na mimi niwe na mpenzi kama wanawake wengine ila siwezi kujiingiza katika mahusiano. Nikifanya hivyo nitakuwa sina tofauti na muuaji.

Mwl. Bashiri:I can’t believe this! Asante sana Mwanaharusi nashukuru kwa upeo wa akili ulionao… Oooh Alhamdulillah!

Mwanaharusi:Sikutaka kuitoa hii siri kwa mtu yeyote ila leo imenilazimu, nakuomba sana unitunzie siri hii, nakuomba sana.

Mwl. Bashiri: Usijali nimekusikia, umenisaidia sana, siwezi kumwambia mtu.

Mwanaharusi:(Anainamisha kichwa chini) Naumia kuishi maisha haya mwalimu.

Mwl:bashiri: Usijali Mwanaharusi, kwa kuwa umeshaniweka wazi mimi nitakusaidia kwa hali na mali.

Mwanaharusi::Nitashukuru mwalimu.

Mwl: Bashiri: Hiyo ndio zawadi nitakayokupa, umenisaidia sana. Angekuwa  mwanamke mwingine angenificha na kuniteketeza.

Mwanaharusi: Sawa nashukuru (Ananyanyuka na kuanza kutoka nje taratibu huku moyoni akiwa na furaha tele. Huku nje Mwanakombo na Mwanawima wanamsubiri Mwanaharusi ili wamwambie kuwa wamemuona akienda kwa mwalimu Bashirii kwa siri…)

Mwanawima: Mapenzi hayana mjuaji, lazima kila binadamu aliyekamilika ayapitie.

Mwanakombo:  Haya tueleze nini kimekusibu mpaka umeamua umkubalie.

Mwanaharusi: Mbona siwaelewi! Nimemkubalia nani? (Anazidi kuwasogelea.)

Mwanakombo: Tumekuona asubuhi na mapema umeingia kwa mwalimu Bashiri hapo hautuelewi nini sasa!

Mwnawima: Najua unataka utufiche ila tumeshajua, tutambulishe tu shemeji yetu.

Mwanaharusi: Heee heeeee, nawashangaa sana! Niliwaambia kwangu

atagonga mwamba.

Mwanakombo:Atagonga mwamba na tumeona umeshanasa…

Mwanawima: Usituchezee akili zetu.

Mwanaharusi:(Anakaa na kupunguza sauti) Mimi ndio Mwanaharusi wa Stonetown (Anajipiga kifua huku akijisifu na kutoa makaratasi mfukoni.)

Mwanakombo:  Haya makaratasi ya nini sasa!

Mwanaharusi:Hivi vyeti nimemlaghai kuwa mimi nimeathirika, nimefika ofisini kwake nikaanza kulia na kumuonesha. Weee!  Alitoa macho huyo kama anataka kukata roho.

Mwanakombo: Yaani wewe kiboko, hiyo akili kakupa nani?.

Mwanaharusi:Hapa hamtaona akinisumbua tena, yaani ananiona kama mkombozi wake.

Mwanawima: Hapo kweli umempatia… Uliwaza nini mpaka ukaamua utumie njia hiyo?

Mwanaharusi:Heeheeee! Wahenga walisema ukitaka kumtibu kichaa anzia pale alipowehukia.

Mwanawima:Una misemo wewe!

Mwanaharusi: Siwezi kumsaliti mama yangu, alinisihi sana kuhusu wanaume.

Mwanakombo:  Hongera ila wewe ni mwanamke mrembo, bado kuna changamoto nyingi sana mbele yako.

Mwanaharusi:Ni kweli lakini ni vyema kuanza kutatua changamoto za sasa, changamoto zijazo zitakuja na suluhisho lake.

Mwanakombo:Sasa ngoja nikupe njia nyingine ya kuwakomesha wanaume wasumbufu.

Mwanaharusi: Enheee niambie shoga!

Mwanakombo:Siku ya kwanza akija mkubalie tu, baada ya hapo anza kumuomba hela.

Mwanaharusi: Nimuombe hela! Akizidai?

Mwanakombo:Hapo ndipo pazuri sasa, akizidisha usumbufu wewe zidisha kumuomba hela.Taratibu ataanza kukata tamaa.

Mwanawima: Mwanzoni atatoa haraka haraka huku akijifariji kuwa mvumilivu hula mbivu, baada ya muda atachoka tu mwenyewe.

Mwanakombo: Tena ukizidi kumuomba hela utaona tu anapunguza kukupigia simu taratibu, maana ataona hizo mbivu zimegeuka kuwa mbichi.

Mwanaharusi: Mmmh! Hapo bado hamjanishawishi, fedha fedheha.

Mwanawima: Jamani mimi naona leo niwaage kabisa, nadhani kuanzia Jumatatu sitaweza kuja skuli na huu mzigo, kila nikipita nahisi kama watu wameanza kuhisi hii hali yangu. Wengine wananiambia nimenenepa sana, siku wakijua si itakuwa balaa! Mimi nitaondoka nitaenda kijijini kwa bibi mpaka nijifungue ndio nitarudi.

Mwanaharusi:Mmh na kweli shoga siku hizi umepata unene wa ghafla, tena shukuru na hayo mavazi yamekusaidia, maana ingekuwa ni shati na sketi ungeshaumbuka.

(Ghafla Mwanawima anaanza kulia kwa uchungu mpaka macho yanakuwa mekundu mithili ya mtu aliyevuta bangi.)

Mwanakombo:Vipi unalia nini tena unaumwa?

Mwanawima: (Anatingisha kichwa hasemi chochote anazidi kulia.)

Mwanaharusi:Tuambie basi unalia nini mbona tulikuwa tunaongea vizuri tu! Au kuna mtu amekukwaza!

Mwanawima: (Anazidi kulia) Kwa nini haya yamenikuta mimi tu, sasa siwezi kuongea vizuri na ndugu zangu, kila mtu ananiona mimi mhuni, kwa nini mimi jamani! Kwa nini?

Mwanakombo:Hilo tu ndio linakuliza! Hebu acha hayo mambo yameshapita.