Sehemu ya Sita A: Usasa Usasambu

Na WILLIAM HIMU

Imepakiwa - Wednesday, July 18  2018 at  16:24

Kwa Muhtasari

Jumbe ni mzee wa makamo mwenye mvi na ndevu nyingi, amekaa kwenye kiti sebuleni anaangalia runinga, watu wote mtaani wanamfahamu kwa busara zake.

 

Sehemu ya Sita A

UTANGULIZI

(Jumbe ni mzee wa makamo mwenye mvi na ndevu nyingi, amekaa kwenye kiti sebuleni anaangalia runinga, watu wote mtaani wanamfahamu kwa busara zake. Pembeni yuko Mwanahawa, Mwinyikheri na Mwanakombo…)

Jumbe:(Anamwambia Mwinyikheri huku akiwa amenuna) Zima hiyo runinga.

Mwinyikheri:Sawa. (Anachukua ‘remote control’ na kuzima.)

Jumbe:Jamani nimekuja hapa lakini nimekuta hali ni tofauti sana!

Mwinyikheri:Hali gani hiyo baba? Kama kuna jambo linakutatiza sema tu mzee wangu.

Jumbe:(Anamuonesha kwa ishara ya mkono atulie) Mimi nimetembea sehemu nyingi lakini haya niliyoyaona hapa sio malezi.

Mwanahawa:(Ametulia anamwangalia.)

Jumbe:Hata msiponiambia niseme nitasema tu…

Mwinyikheri: Mmmh! (Wanaangaliana na mkewe.)

Jumbr:Juzi nilivyofika hapa, mara tu baada ya kunipokea nikaona kila mtu anaendelea kuperuzi kwenye simu yake. Hata muda wa kumlaki mgeni hamna! Yaani hata haka katoto kana simu?

Mwinyikheri:Mambo ya utandawazi hayo mzee, inatulazimu tufanye hivyo… Sasa dunia ipo kiganjani.

Jumbe:Ahaaaa! Utandawazi enee! Jana usiku mzima nimemsikia anaongea na simu badala ya kuutumia muda huo kujisomea, huo ndio utandawazi?

Mwinyikheri: Hapana mzee.

Jumbe:Usimpe mtoto uhuru kupita kiasi. Uhuru bila mipaka ni uwendawazimu. Kila kitu kina wakati wake.

Mwinyikheri: Nimekuelewa mzee, nisamehe nitalifanyia kazi.

Jumbe: Ni nani aliyemnunulia hii simu! Mtoto muda wote simu sikioni kama dalali wa viwanja na nyumba?

Mwanahawa: (Kimya Anatikisa kichwa)

Mwinyikheri: (Kwa kusitasita) Ni mimi baba ila nitayamaliza mzee wangu! Nimekuelewa!

Jumbe:  Huu ni upuuzi! Sitaki nimuone na simu tena. Hebu tazama alivyokosa adabu, naongea bado tu anaendelea kuchezea simu.  Kwenu ninyi maendeleo ni kuwapa watoto wadogo vitu vinavyochangia kuvuruga bongo zao?

Mwinyikheri:Sio hivyo baba

Jumbe:Sio hivyo nini weweee, kimya! Tatizo lenu vijana wa siku hizi mnawadharau sana wazee wenu, lakini hamjui kuwa kinywa cha mzee kinanuka ugoro lakini hakisemi uongo.

Mwanahawa:Ni kweli baba, mimi nilisema sana lakini sikusikilizwa, hata kazi za nyumbani hafanyi tena.

Jumbe: Kumnunulia simu sio kumpenda, nendeni kijijini muangalie watu wanavyoteseka. Huku hela mnachezea tu, pesa maua mwanangu.

Mwinyikheri:Nimekuelewa baba nitalifanyia kazi.

Jumbe: Yule rafiki yake aliyekuja jana huku akiwa analia amepata ujauzito.Yote haya ni haya mambo yenu ya usasa. Michezo mingi michafu watoto wanajifunza mtandaoni.

Mwanahawa:Heee, Mwanawima ana mimba? Haya na wewe endelea kuhangaika tu utapata unachokitafuta, si ndio rafiki yako mkubwa yule.

Jumbe:Ana mimba kubwa tu…

Mwinyikheri:  Mmmh! Anachokihangaikia binadamu ndicho Allah anachompa, yeye kachagua mimba.

Mwanahawa:  Usiseme hivyo na wewe umezaa. Hawa watoto wako kwenye kipindi kigumu. Ni lazima waongozwe katika misingi sahihi ili kukabiliana na hawa wakware.

Mwinyikheri:Wakati mwingine mtoto ukimfuatilia sana unamharibu lakini pia unakuwa unamnyima uhuru wa kuweza kujua ulimwengu unavyokwenda.

Jumbe:Zamani maisha yalikuwa ya upendo sana.  Mgeni alipofika nyumbani, watu wote waliacha kazi zao na kujumuika naye. Ilikuwa ni nadra sana kumkuta mtoto wa kike kasimama na mwanamume. Utamaduni huu ulianza kubadilika taratibu kadri muda ulivyozidi kwenda. Watu walianza kubadilika kwa madai kuwa wanakwenda na usasa. Sayansi na teknolojia ikawa imezalisha n’ge mwenye sumu kali kwa vijana wetu. Badala ya simu zitumike kuleta maendeleo imekuwa ni kinyume. Zimesasambua kila kitu na kutuacha watupu. Jadi tuliyojivunia kizazi hadi kizazi imebaki ni simulizi.  Hakuna heshima tena wala subra yenye heri. Zamani wanawake walikuwa wanajisitiri,   walikuwa na haya, siku hizi wamekosa haya. Tunaona mpaka nguo zao za ndani. Wanamtangazia nani hiyo biashara! Wameyaona wapi haya na kuyaiga? Mitandaoni! Sayansiusasa imezidi kuwasasambua kila kukicha. Haya sio malezi ni hatari, ni hatari kabisa…

 

(Asubuhi Mwanakombo anajiandaa kwenda skuli baba yake anamuwahi mlangoni.)

Mwinyikheri: Hebu nipe hiyo simu yako…

Mwanakombo: (Anashtuka kwani bado kuna picha na jumbe mbalimbali alizotumiwa usiku) Aaah ipo ndani.

Mwinyikheri: Ndio, ilete sasa hivi (Anakaza sura.)

Mwanakombo: (Anatetemeka kwa hofu) Mimi nachelewa skuli.

Mwinyikjeri:Nasema kailete sasa hivi, (Anatoka barazani na kumuita mkewe.)

Mwanakombo: (Anaingia chumbani kwake na kutoka na simu) Hii hapa baba.

Mwinyikheri:(Anamuita mkewe huku akiwa anaendelea kuiwasha simu) Mwanahawa! Mwanahawaaaaaa.

Mwanahawa:Abee mume wangu.

Mwinyikheri:Samahani kaa kidogo hapa.

Mwanahawa: Nafanya usafi huko nje.

Mwinyikheri: Hamna shida dakika tatu tu, vipi baba bado amelala?

(Kwa sauti ya chini.)

Mwanahawa:Ndio.

Mwinyikeri:Nimeamua nimpokonye mwanao hii simu ili baba atulie, hebu kaitunze.  (Anasita kumpa anaifunguaupande wa ujumbe mfupi) Mmmh! mke wangu haya mazito (anamsogezea mkewe asome).

Mwanahawa: Sasa ona huu uchafu, hayo ndio uliyokuwa unayataka mume wangu.