Sehemu ya Sita B: Usasa Usasambu

Na WILLIAM HIMU

Imepakiwa - Wednesday, July 18  2018 at  16:25

Kwa Muhtasari

Teknolojia inaweza kuzua migogoro katika jamii isipotumiwa kwa tahadhari kuu.

 

(Baada ya wiki mbili Mwanawima anaaza kwenda skuli japo kwa kujikongoja.. Asubuhi Mwl. Bashiri anaingia darasani na fimbo yake mkononi huku amekasirika kama faru.)

Mwl. Bashiri: (Anagonga mlango kwa fimbo wanafunzi wananyamaza)

Kiongozi wa darasa yuko wapi?

Wanafunnzi: Leo hajafika.

Mwl. Bashiri: Haya Mwanaharusi kusanya daftari zote ulete ofisini.

(Mwanawima na Mwanakombo wanaangaliana kisha wanatabasamu, baada ya Mwl. Bashiri kutoka wanatoa kicheko kwa sauti mpaka darasa zima wanageuka.)

Mwanakombo: (Ananong’ona) Alijifanya mjanja leo kapatikana hatoki leo hata kwa hirizi…

Mwanawima: (Kwa sauti ya chini) Lakini huu anaoufanya mwalimu Bashiri ni ukatili.

Mwanakombo:Nyamaza wewee, ukatili ndio unaujua leo! Jambo usilolijua ni sawa na usiku wa giza.

Mwanawima: Hata kama, ila tambua kuwa mapenzi hayalazimishwi.

Mwanakombo:(Anamkazia macho) Sasa nani kalazimishwa hapo

Mwanawima: (Kimya)

Mwanakombo: Akirudi nitamshauri aache ujinga, yule mwalimu ana hela. Pale anaua ndege wawili kwa jiwe moja. Huku anafaulu mitihani kule anapata hela za kutosha…

Mwanawima: Hebu tuachane na hayo shoga, kitumbo ndio hichoo kimeanza kuonekana nitauweka wapi uso wangu?

Mwanakombo:  Mimba kwa mwanamke ni kama samaki na maji, ingekuwa mimba hiyo kaipata mwanamume ndio ingeshangaza lakini kaipata mwanamke ajabu nini hapo?

Mwanawima: Hapana Mwanakombo usiseme najisikia

aibu sana, lakini nashukuru sijatoa mimba maana hivyo

vitisho alivyotupa daktari ni hatari, kumbe watu  wanaweza

kufa wakitoa mimba!

Mwanakombo:  Hizo hadithi tu, tungelikuwa hatutoi

mimba dunia ingeshajaa watu siku nyingi.

Mwanawima: (Anacheka kwa kujilazimisha) Heee heeee, una maneno wewe!

Mwanakombo: Looh! Nishindwe vyote lakini hata

kuongea? Kuongea ndio jadi yetu.

Mwanawima:Ila mimi nimeyaona madhara ya kutoa mimba kwa watu wengi ndio maana napata hofu.

Mwanakombo: Huo uwoga wako tu!

Mwanawima:Nini! Tena ngoja nikuambie kitu. Mimi kuna siku nilienda kwa dada, ilivyofika jioni ya saa kumi hivi akaja rafiki yake akiwa analia huku akigaragara chini. Damu nyingi zilikuwa zinamtoka. Dada alipomuuliza ana tatizo gani, alisema kuwa ametoa mimba kwa siri. Alizidi kuchoka mpaka akazirai ndipo tulipomwahisha hospitali. Aligundulika kuwa alitoa mimba ila vipande vilibaki tumboni. Daktari alijitahidi kumtibu na kufanikiwa ila hakuweza kuzaa tena kwa kuwa kizazi kiliharibika vibaya.

Mwanakombo:Heee! Kumbe mambo ndio yanakuwa hivyo?

Mwanawima:Ndio, ni hatari sana ndio maana napata hofu.

Mwanakombo:  Ila hao walitumia njia za panya, wangeenda kwa wataalamu, wanatoa mimba bila kuumwa hata kichwa…      

(Wakiwa bado wanaongea kwa siri Mwanaharusi naye anamaliza kukusanya madaftari, anabeba kwa unyonge na kuelekea ofisini kwa mwalimu huku mapigo ya moyo yakimwenda mbio.)

Mwl. Bashiri:Vizuri, weka hapo juu ya meza (Anatabasamu.)

Mwanaharusi:Sawa (Anaweka na kugeuka kutaka kuondoka)

Mwl. Bashiri: Bado, subiri unaenda wapi?

Mwanaharusi:Bado nini mwalimu (Woga unazidi.)

Mwl. BAashiri: Mwanaharusi (Anamwita na kumuonesha kwa ishara akae kwenye kiti.)

Mwanaharusi:Abeee (Anaelekea kukaa kwenye kiti alivyoelekezwa)

Mwl. Bashiri: Hapa ondoa woga, tunaongea kama marafiki na sio kama mwalimu wako tena. Ualimu ni huko darasani.

Mwanaharusi:(Kimya, anaangalia chini)

Mwl. Bashiri: Nimekueleza hisia zangu muda mrefu lakini sikuelewi, unataka tuwe tunakimbizana kama watoto vichochoroni?

Mwanaharusi:Mwalimu, mimi naogopa, nafikiria utu wangu na thamani yangu. Wazazi wangu hawatanielewa. (Anainamisha kichwa chini kwa woga.)

Mwl. Bashiri: Utu na thamani ipi ambayo nitaiondoa kwako? Wewe ni mrembo Mwanaharusi lazima uwe na mtu kama mimi. Usihangaike na hao wanafunzi wenzako watakuharibia maisha.

Mwanaharusi: Mimi siwezi…

Mwl. Bashiri:Kidato cha nne wewe ni dada kabisa lakini unakuwa muoga kama mtoto.  Kwa hiyo uko tayari kufeli kuliko kunisaidia mwalimu wako?

Mwanaharusi: Hapana mwalimu, napenda sana nifikie malengo yangu, siwezi kuchanganya mambo mawili kwa wakati mmoja. Nitashindwa!

Mwl. Bashiri: Haya wewe nenda ila tambua kuwa maisha yako ya hapa skuli yapo mikononi mwangu.

 Mwanaharusi:Sawa mwalimu nipe muda kidogo mpaka kesho asubuhi nikifika skuli nitakujibu.

Mwl. Bashr:Sio utanijibu sema utanikubalia.

Mwanaharusi: Sawa, nimekuelewa!

Mwl. Bashiri: Chukua hela ya soda (Anampa noti ya elfu tano.)