http://www.swahilihub.com/image/view/-/4890032/medRes/2194553/-/xcsjbwz/-/maria.jpg

 

Maandishi ikiwemo sababu zinazochochea uundaji wa istilahi za Kiswahili

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  10:58

Kwa Muhtasari

  • Kwa mujibu wa Kamusi ya Karne ya 21, istilahi ni "msamiati wa uwanja fulani maalum" (Kamusi ya Karne ya 21, uk 154)
  • Baadhi ya sababu zinazochochea uundaji wa istilahi za Kiswahili ni msukumo wa ugunduzi na msukumo wa kuingiza maarifa mapya katika lugha kutoka lugha nyingine

 

UPO muundo wa maandishi unahusisha alama moja kwa neno moja (characters) jinsi ilivyo hadi leo kwa mfano katika lugha ya Kichina.

Tukiachana na muundo huo, kuna matumizi ya alfabeti.

Manufaa ya herufi za alfabeti ni ya kwamba alama chache tu zinatosha kwa kuandika lugha yote.

Kwa mfano katika maandishi ya Kichina mwanafunzi anahitaji kujifunza alama chungu nzima kabla hajaanza kuandika chochote.

Baadhi ya herufi zinazotumiwa zaidi ulimwenguni ni zile za alfabeti na kilatini. Katika nyanja za kimataifa alfabeti zinazotumiwa kwa wingi ni alfabeti za Kiarabu na alfabeti za Kikirili.

Herufi hizi zinatofautiana kwa jumla ingawa kuna pia herufi zinazofanana katika kundi la alfabeti. Kwa mfano alfabeti za Kilatini na Kikirili zote zimetokana na alfabeti ya Kigiriki.

Aidha, alfabeti ya Kiarabu ina herufi za nyongeza ikitumiwa kwa kuandika lugha kama vile Kiajemi, Kiurdu na kadhalika.Hata hivyo, mchakato wa uundaji wa maneno au istilahi katika Kiswahili umekuwa safari yenye misukosuko kutokana na sababu mbalimbali. Jinsi anavyoeleza Mwanasoko na wenzake: 1992:22 “Uundaji wa kudhamiria wa istilahi za Kiswahili ambao umekuwa ukiendelea tokea mwaka 1930 umekuwa ukikabiliwa na matatizo anuwai na hivyo kuufanya usiwe na mafanikio ya kuridhisha. Matatizo hayo, yanajumuisha upungufu mkubwa wa istilahi katika takribani nyanja zote za taaluma; mparaganyiko wa baadhi ya istilahi unaosababishwa na misingi potofu... ya uundaji wa istilahi”

 

Sababu zinazochochea uundaji wa maneno katika Kiswahili

Kwa mujibu wa Sager 1990:80, Uundaji wa istilahi katika Kiswahili ulichochewa na misukumo ya aina mbili:

i. msukumo wa ugunduzi

ii. msukumo wa kuingiza maarifa mapya katika lugha kutoka lugha nyingine

Msukumo wa Ugunduzi

Katika hali hii, aghalabu istilahi huundwa na wagunduzi kinasibu.

Uundaji istilahi kwa ajili ya kuingiza maarifa katika lugha

Hali hutokea au hutekelezwa kwa kudhamiria na huzingatia kanuni mahususi. Uundaji huu huhusisha lugha mbili:

Lugha chanzi - lugha ya jamii yanakotoka maarifa

Lugha lengwa -  lugha ya jamii inayopokea maarifa

Katika somo linalofuata, tutasoma kuhusu msukumo wa kuingiza maarifa mapya katika lugha kutoka lugha nyingine.

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo

Masebo, J. A. (2010). Nadhari ya Lugha Kiswahili 1.Dar es Salaam: Nyambari Nyangwine Publisher.

Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.

Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiko, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi Kenya: Longhorn Publishers

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com