http://www.swahilihub.com/image/view/-/4895246/medRes/2197876/-/1a5cf1z/-/wangari.jpg

 

Uundaji wa maneno au istilahi katika lugha ya Kiswahili

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  10:58

Kwa Muhtasari

Uundaji wa maneno unarejelea kuhusu mchakato wa mabadiliko ya istilahi na muundo unaosababishwa na mabadiliko ya sayansi na tekinolojia ya kila uchao katika nyanja mbalimbali za jamii.

 

KATIKA makala ya leo, tutaanza kuchambua na kupambanua dhana ya uundaji wa maneno katika Kiswahili.

Tutaishughulikia mada hii tukidhamiria kujibu swali la msomaji wetu Silvanous Kunga na wengineo.

Uundaji wa Maneno

Uundaji wa maneno unarejelea kuhusu mchakato wa mabadiliko ya istilahi na muundo unaosababishwa na mabadiliko ya sayansi na tekinolojia ya kila uchao katika nyanja mbalimbali za jamii.

Istilahi ni neno linalowakilisha dhana fulani katika uwanja maalumu wa maarifa mathalan kisiasa, kiuchumi na kadhalika.

Kwa mujibu wa Matinde (2012), uundaji wa maneno hutekelezwa ili kukidhi dhima ya lugha kama chombo kinachojitosheleza katika mawasiliano.

Kwa mantiki hii, ili kukidhi haja hii kuna mbinu anuai zinazotumika katika uundaji na ukuzaji wa istilahi ya maneno katika lugha ya Kiswahili.

Uundaji wa maneno unaweza pia kufafanuliwa kama ujenzi, uzalishaji au utengenezaji wa maneno mapya. Uundaji wa maneno mapya husaidia kuongeza msamiati katika lugha ili kukidhi mahitaji ya mawasiliano.

Uundaji wa maneno mapya husababishwa na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na maendeleo ya kisayansi yanayotokea katika jamii. Kwa mfano, kutokana na masuala ibuka, kuna maneno chungunzima ambayo yameibuka na yanayotumika katika jamii mathalan; ukeketaji, ruwaza, tovuti, miundomsing, ujasiriamali miongoni mwa mengine kutokana na mabadiliko ya kijamii.

Ni vyema kuelewa kwamba undaji wa maneno hubadilisha maana ya maneno asili.

Kuna mbinu mbalimbali za uundaji wa maneno au ukipenda istilahi jinsi zilivyoorodheshwa ifuatavyo:

i. Kutohoa maneno ya lugha nyingine

ii. Kubadili mpangilio wa herufi

iii. Kuambatanisha maneno.

iv. Uambishaji wa maneno

v. Kusanifisha sauti, umbo, mlio na sura

 

Herufi inamaanisha alama katika mwandiko unaofuata alfabeti. Ni vyema kufahamu kwamba kila herufi ni alama ya sauti au fonimu fulani mathalan A,B,C,D.

Lugha za kwanza zinazojulikana kama vile Kigiriki na Kifinisia zilitumia mtindo huo.

Aidha, miandiko iliyotangulia muundo huu ilikuwa na alama moja kwa silabi maarufu mwandiko silabi.

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

 

Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.

Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiko, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi Kenya: Longhorn Publishers.

Rubanza,Y. I.(1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania

 

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com