http://www.swahilihub.com/image/view/-/4895246/medRes/2197893/-/1a5cdcz/-/wangari.jpg

 

Uundaji wa maneno kwa madhumuni ya kuongeza maarifa katika lugha

Mary Wangari

Mwandishi Mary Wangari. Picha/MAKTABA 

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  12:29

Kwa Muhtasari

Kazi huanza kwa kukusanya istilahi katika lugha chanzi, kufafanua dhana zinazobebwa na istilahi na kisha kuziundia visawe katika lugha lengwa.

 

KATIKA uundaji wa istilahi kwa madhumuni ya kuingiza maarifa katika lugha, kazi huanza kwa kukusanya istilahi katika lugha chanzi, kufafanua dhana zinazobebwa na istilahi na kisha kuziundia visawe katika lugha lengwa.

Kwenye utaratibu huu, uundaji wa istilahi huwa wa mtindo wa faharasa au wa kamusi ya istilahi ya lugha mbili.

Mtindo huu wa kuunda istilahi hutumika hasa kwa lugha zinazoendelea kama juhudi mojawapo ya kuziwezesha lugha hizo kupokea maarifa ya sayansi na teknolojia kutoka lugha zilizokomaa na kubobea katika maarifa hayo.

Uundaji wa istilahi za Kiswahili hufanywa zaidi kwa mtindo huu ambapo kazi huanza kwa kukusanya istilahi kwa mfano katika Kiingereza, kisha kuziundia visawe vya Kiswahili na wakati mwingine kutoa fasili za dhana za istilahi husika.

Kwa mujibu wa Baraza la Kiswahili (BAKITA) Hadi sasa juhudi za uundaji wa istilahi za Kiswahili hazijaonyesha mafanikio ya kuridhisha. Baraza hili ambalo kisheria ndilo lenye mamlaka ya kuratibu shughuli za uundaji wa istilahi za Kiswahili, hadi sasa limeweza tu kuandaa na kuchapisha faharasa kadha za istilahi na halijachapisha kamusi za istilahi za fani maalumu.

Isitoshe, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki), zamani ikifahamika kama Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hujihusisha na utafiti na ukuzaji wa istilahi za Kiswahili na hadi sasa imeweza kuchapisha kamusi za istilahi za fani za Fizikia, Kemia, Biolojia, Lugha na Isimu, Historia, Tiba, Biashara na Uchumi, na Sheria.

Hata hivyo, kamusi hizo nyingi ni ndogo ndogo, ambapo Kamusi ya Historia (2004) yenye kurasa 35 pekee ndiyo ndogo kabisa huku Kamusi ya Tiba (2003) yenye kurasa 292 ikiwa ndiyo kubwa.

Kamusi nyingine ni Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha (2004) yenye kurasa 118; Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (1990) yenye kurasa 58; Kamusi ya Biashara na Uchumi (1999) kurasa 78; Kamusi Sanifu ya Biolojia, Fizikia na Kemia (1990) kurasa 217; na Kamusi ya Sheria (1999) yenye kurasa 116.

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo:

Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Natharia. Kwa Sekondari, Vyuo Vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.

Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiko, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi Kenya: Longhorn Publishers.

Rubanza,Y. I. (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com