http://www.swahilihub.com/image/view/-/2605040/thumbnail/932770/-/20l30pz/-/bendi+flv.jpg

 

Bendi ya T 412 yaelezea usanii wake wa injili

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Wednesday, January 28  2015 at  15:47

Kwa Muhtasari

Ni kikundi kinachonuia kutoa ushindani mkali kwa bendi ambazo zimekuwa zikivuma nchini katika kipindi cha hivi majuzi, lakini tofauti ni kuwa azma yao kuu ni kueneza injili.

 

NI KIKUNDI kinachonuia kutoa ushindani mkali kwa bendi ambazo zimekuwa zikivuma nchini katika kipindi cha hivi majuzi, lakini tofauti ni kuwa azma yao kuu ni kueneza injili.
Wanafahamika kama T412 kundi linalojumuisha wasanii Jemedy, Clive, Milome, Fortunate (42n8) na Muhanji. Jina la bendi hii linatokana na kitabu cha Biblia cha 1 Timotheo 4:12, kinachowahimiza vijana
kutoogopa kuhubiri neno kutokana na umri wao mdogo, na badala yake kuwa mfano kwa Wakristu wa kila umri.
Kufikia sasa wana zaidi ya nyimbo tano  ambazo zinazidi kupata umaarufu, huku wakiwa katika juhudi za kurekodi kanda yao ya tatu ya mseto kwa usaidizi wa kampuni ya kurekodi muziki ya  BoxHouse Media.
Katika mahojiano wanaeleza kuhusu historia ya kikundi hiki ambacho kwa kwengi ni geni, vile vile jitihada zao za kuthibitisha muungano wao na kudumisha ujumbe wa injili katika kila kibao wanaochotunga.
SWALI: Sio wengi wanaofahamu muziki wenu. Elezeni kwa kina aina ya nyimbo mnazotunga.
JIBU:  Sisi hurekodi muziki wa injili lakini hatuna mipaka kuhusu mdundo wa muziki tunaorekodi.
SWALI: Mlikutana wapi?
JIBU: Tulikutana katika Kanisa la (Citam BuruBuru) tukiwa bado wanafunzi wa shule ya upili ambapo tulikuwa tunashiriki katika koregrafia nyakati za likizo. Wakati huo tulikuwa tunajiita Revolutionized na tulikuwa hasa tunahusika na masuala ya densi. Mwaka wa 2011 tulijizindua rasmi kama kikundi cha densi lakini wengi wetu
walilazimika kuondoka kutokana na shughuli za kimasomo na mambo mengine. Mwanzoni tulikuwa wasanii 30 kabla ya wengine kwenda na hapo tukasalia wanne ambapo Jemedy aliungana nasi mwaka wa 2012.
SWALI: Tuelezeni mengi kuhusu kazi yenu kufikia sasa?
JIBU: Tuna kanda mseto mbili kila moja ikiwa ni vibao 15. Zinajumuisha ‘Revive- All’ iliyozinduliwa mwaka wa 2012, ‘Good News’ tuliyoitoa mwaka jana na kwa sasa tunashughulikia mkusanyiko mpya tunaotarajia kuzindua mwaka huu.

Kanda hii ina vibao kama vile ‘Aon Know’ na ‘We Deh’ miongoni mwa nyimbo zingine.
SWALI: Kutokana na umaarufu wa bendi kadha mfano Sauti Soul, huenda wengi wakadhani kuwa umekuwa mtindo kwa wanamuziki kukusanyika kwa vikundi. Kwenu pia ni hivyo?
JIBU:  La! Tulipoanza hatukuwa na kikundi maalum ambacho tungeweza jilinganisha nacho. Ni kweli kuwa huu umekuwa mtindo lakini mwanzoni tulijaribu kufanya kazi kama wanamuziki binafsi lakini kwa kikundi,
mfano wa bendi ya Amerika ya Amerika la 116 Clique, bila mafanikio. Ni hapa ndipo msanii  Ngalizo Mtukawaida wa bendi ya Yunasi ambaye pia ni produsa wetu alitushauri kuwa tungefanya vyema kama bendi.
SWALI: Mnapata wapi maono ya kuandika nyimbo zenu?
JIBU: Msukumo wetu hasa unatoka kwa Mungu, Biblia, maisha na ushuhuda wa watu wengine.
SWALI: Kama nilivyotaja awali, idadi ya vikundi vya muziki vinavyovumbuliwa kila siku vinaonegezeka kila mara. Mnadhani kuwa kuna msukumo wa kufanikiwa kama bendi zingine mfano Yunasi au Sauti Sol?
JIBU: Msukumo wa kufanikiwa maishani unamkumba kila mtu lakini tunachofahamu ni kuwa kuna msimu na wakati wa kila jambo chini ya mbigu.
SWALI: Ni kawaida kuwapata wasanii wengine hasa hapa nchini wakifanya mambo mengine kando na muziki ili kujiendeleza kimaisha. Kwenu muziki ni kila kitu?
JIBU: La! Mbali na muziki tuna maisha, kwa mfano Jemedy ni mwanafunzi na mfanyabiashara, Muhanji ni mhariri mbunifu na podusa wa video, Milome ni mwanafunzi na mtaalamu wa masuala ya kompyuta, Clive ni msanii na produsa.
SWALI: Wasanii wengi wa injili husema kuwa kueneza injili ndio dhamira yao kuu. Je kuuza kanda au sidii kuna umuhimu kwenu?
JIBU: Ni kweli kuwa nia yetu kuu kama wasanii wa injli ni kueneza neon lakini pia kuuza rekodi kuna umuhimu kwani hutufadhili kujiendeleza kimuziki. Hata Biblia kupitia kitabu cha Wahubiri inasema kuwa pesa husuluhisha matatizo yote.
SWALI: Baada ya kujiweka imara mngepena kufanya kazi na wasanii gani?
JIBU: Orodha hiyo ni ndefu lakini hapa nchini tunatamani sana kufanya kazi na Jemimah Thiongo, Echo Dydda, Recapp, Rekindle Flame,Kamlex, Samukat,Sulwe, Span One na Juliani miongoni mwa wengine.

Kimataifa tungependa kushirikiana na kikundi cha 116 clique, RPSMG, Papa San, Sherwin Gadner, Dj Nicholas na Mouthpiece kati ya wengine.