http://www.swahilihub.com/image/view/-/2605068/thumbnail/932791/-/mhcnxvz/-/cink+flv.jpg

 

DJ Cink aelezea usanii wake

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Wednesday, January 28  2015 at  16:12

Kwa Muhtasari

Ni miaka minne sasa tangu ajitose rasmi katika ulingo wa kuwa dijei na tayari ameingia katika orodha ya madijei wanaovuna vinono kutokana na kazi hii ambayo kwa miaka imekuwa ikihusishwa na uhuni.

 

NI MIAKA minne sasa tangu ajitose rasmi katika ulingo wa kuwa dijei na tayari ameingia katika orodha ya madijei wanaovuna vinono kutokana na kazi hii ambayo kwa miaka imekuwa ikihusishwa na uhuni.


Lakini kwa Jeff Kitili al-maarufu Dj Cink hii ni kazi kama ingine yoyote kwani imemwezesha kujikimu kimaisha na kulinda familia yake changa bila tatizo.


Kwa mwezi kazi hii inamwezesha kuunda kati ya Ksh 50,000 na Ksh 100,000 kulingana na jinsi mwezi ulivyo, vile vile kuambatana na msimu.


“Kwa mfano msimu wa sherehe kama mwezi uliopita mambo huwa mengi ni wakati huu ambapo mapato pia huongezeka,” aeleza.


Kazi zake nyingi zinahusisha mialiko ya makampuni, vlabu na hata mialiko ya kibinafsi kama vile kuburudisha katika sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa.


“Malipo ya kuburudisha katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa hufikia Ksh 30,000, huku malipo ya kutumbuiza klabuni ikiwa kati ya Ksh 15000 na Ksh 20,000 kwa usiku,” aeleza.


Jina lake limechochewa na pendo lake pia kwa masuala ya jikoni kwani mbali na muziki, anapenda upishi hasa kutokana na sababu kuwa amesomea masuala ya usimamizi wa hoteli.


“Kabla ya kuamua kujiita Dj Cink, nilijaribu majina tofauti yanayohusiana na jikoni ikiwa ni pamoja na dj spoon, dj sufuria lakini hayakunipendeza na hapo ndipo nilipofikiria jina la Sink yaani sinki, ila tu nikabadilisha herufi ya S na kuwa C,” asema.


Amerekodi mchanganyiko wa muziki kadha huku baadhi ya kanda mseto zake zikiwa pamoja na ‘Sitolia 1’ na ‘Dancehall vol 1-3” miongoni mwa kazi zingine.
Ari yake ya kuwa dijei ilitokana na Dj Trace, dijei mzaliwa wa Uingereza na ambaye kazi yake inatambulika ulimwenguni kote.

“Naweza mtazama usiku kucha bila kuchoka kutokana na ujuzi wake wa kipekee katika uchanganyaji wa muziki mbali mbali,” aeleza.


Hapa Kenya ari yake ya kuwa dijei imechangiwa na madijei kama vile Dj Prince mbali na Dj Adrian.

Kabla ya kufika alipo sasa, Dj Cink anasema alianza kufanya kazi katika klabu ndogo mtaani kama mbinu ya kupiga msasa kipaji chake.

Kabla ya DJ kuwasili
“Kutokana na sababu kuwa kazi haikuwa nyingi mtaani, niliamua kuendeleza kazi yangu kati kati mwa jiji la Nairobi na hasa katika klabu ya Trends Pub, ambapo ningecheza kati ya saa tisa alasiri na saa kumi na mbili jioni kabla ya dijei kuwasili.


Kulingana naye hapa hakupata mwangaza kama alivyotarajia na hapo akaamua kuhama tena  na kutafuta kazi kwa klabu ya Genesis club, ambapo alipata fursa ya kutumbuiza kuanzia saa nane alfajiri hadi asubuhi.


Akiwa hapa nyota yake iling’aa na haikuwa mua kabla ya kupata mwaliko wa kufanya kazi katika kituo kimoja cha redio hapa jijini.


“Nilifaidika sana mwezi jana kwani nilipata mialiko nyingi na naamini kuwa ilikuwa kutokana na mfichuo niliopata kupitia redioni,” aeleza.


Hata hivyo hii haimaanishi kuwa hajadhurika na changamoto zinazoambatana na kazi hii kama vile dhana potovu inayowaonyesha madijei kuwa wahuni na waliolemewa kimasomo.

Penzi la kazi limepiku masomo
“Baadhi yetu tumesoma ila tu ni kuwa penzi letu kwa kazi hii limepiku mambo tuliyosomea,” asema.


Kadhalika kuna tatizo la kutumiwa vibaya na baadhi ya wateja walio na mazoea mabaya ya kukwepa kulipa hata baada ya kufanyiwa kazi.

“Ili kukabiliana na tatizo hili ni vyema kuitisha kiwango fulani cha pesa kabla ya kuanza kazi,” aeleza.


Kando na hayo alalamikia tatizo la kupotea kwa umeme unapohitajika kufanya kazi.


Kwa wale wanaotamani kuingia katika ulingo huu, Dj Cink asema sharti uwe na ufahamu kuhusu aina tofauti za muziki, mbali na kutia bidii na kuwa na nidhamu.
“Nidhamu itamwezesha Dj kuwa kuwasili kwa wakati ufaao anapohitajika kufanya maonyesho,” aeleza.


Mbali na hayo, asema sharti uwe na mazoea ya kufanya mazoezi kila mara kwani vifaa vinavyotumika katika fani hii hufanyiwa mabadiliko kila mara.
Mipango yake ya siku za usoni ni kufungua chuo chake cha kutoa mafunzo maalum ya udijei.