http://www.swahilihub.com/image/view/-/2605086/thumbnail/932809/-/gny9qmz/-/viola+flv.jpg

 

Viola aelezea usanii wake wa mtindo wa chakacha

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Wednesday, January 28  2015 at  16:44

Kwa Muhtasari

Mtindo wake wa kuimba unaohusisha muziki wa Chakacha, uko mbioni kumweka miongoni mwa wanamuziki mahiri nchini.

 

MTINDO wake wa kuimba unaohusisha muziki wa Chakacha, uko mbioni kumweka miongoni mwa wanamuziki mahiri nchini.
Ni suala ambalo Viola Karuri asema linampa nguvu akilinganishwa na wasanii wengine hasa ikizingatiwa kuwa sio wanamuziki wengi wa kisasa
wanafuatilia midundo ya kiasili.
Licha ya kuwe pengine sio wasanii wengi wanaofahamu amekuwa katika sekta hii kwa takriban miaka sita ambapo alirekodi wimbo wake wa
kwanza “Everything” mwaka wa 2009.

“Kibao hiki kinazungumzia bidii na nguvu nilizotumia kutunga na kurekodi wimbo huu ambao ulinichukua muda,” aeleza.
Mwaka jana, alizindua kibao cha kwanza katika albamu yake ya pili “Aibu (Out The Door)”, wimbo uliofuatiwa na kombora lake la hivi majuzi, “Milele”, ambapo amemshirikisha mwanarepa Collo.

“Ni kibao ambacho kinazidi kupata umaarufu miongoni mwa mashabiki,” aeleza.
Japo bado yungali anatokota kwenye chungu cha muziki, tayari amepata fursa ya kufanya maonyesho na baadhi ya wanamuziki maarufu kama vile Jonathan Butler, Lalah Hathaway na Abraham Laborel.
Mbali na kipaji chake kimuziki, uimbaji wake umetiwa nakshi na mafunzo ya muziki aliyopokea katika Chuo cha muziki cha Berklee nchini Amerika
ambapo alihitimu na shahada ya muziki na uhandisi wa sauti miaka kumi iliyopita.
SWALI: Wasanii na wanamuiki wengi watajika hawakusomea muziki. Unadhani kuwa masomo yako katika nyanja hii yameimarisha kipawa chako
kimuziki?
JIBU: Kwangu mimi masomo katika chuo cha Berklee yalinisaidia kuimarisha kipawa changu na pia kunifungulia milango ya kupata fursa
ambazo nisingeziona iwapo singejiunga na taasisi hiyo. Kwa ufupi kipaji changu kiliimarika sana na mafunzo niliyopokea.
SWALI: Nimepata fursa ya kusikiza nyimbo zako kadha na ukweli ni kuwa utunzi wako una athari za utamaduni wa sehemu za pwani ya Kenya. Una
asili huko?
JIBU: Nyimbo zangu nyingi zina ushawishi wa tamaduni za Kiswahili kwani niliwahi ishi Mombasa, mbali na kuwa nina asili ya Tanzania.
SWALI: Muziki wako unahusisha mdundo wa chakacha. Nani hasa alikupa moyo wa kuimba muziki huu hasa ikizingatiwa kuwa haufuatiliwi sana na
wanamuziki wa kizazi cha sasa?
JIBU: Kiwango cha jinsi unavyofasiri ujumbe kwenye muziki kina uwezo wa kuimarisha au kukatiza jinsi unavyomakinika.

Midundo ya Afrika inaendelea kutawala jukwaa la ulimwenguni kote kumaanisha kuwa kuna rasilimali nyingi katika muziki wa kiasili na pengine nilipata mvuto hapa.

Muziki wa chakacha ni sehemu ya utamaduni wetu na iwapo utarekodiwa vyema yaweza pendeza na kuvutia hata wasio na ufahamu kuhusu mdundo huu.

Ukipata nafasi jaribu kusikiza kibao Y.O.LO. (You Only Live Once) na utafahamu ninachosema.
SWALI: Umepata fursa ya kuishi katika dunia mbili, Amerika na hasa jijini New York na hapa Kenya. Kuna tofauti gani kati ya sehemu hizi mbili hasa kimuziki?
JIBU: Mahitaji na midundo ni tofauti lakini kwa kweli aina tofauti ya muziki vile vile viwango vya muziki vinakaribiana.

Pengine tofauti kuu ni kuwa nchini Amerika muziki unapatikana kwa urahisi kumaanisha kuwa mfumo wao wa usambazaji muziki ni imara huku mialiko ya kufanya maonyesho ikipatikana kila mara.
SWALI: Ulihisi vipi kuimba katika jukwaa moja na baadhi ya wanamuziki watajika kama vile Jonathan Butler?
JIBU: Mwanzoni nilikuwa na uoga hasa ikizingatiwa kuwa sikutarajia. Lakini baada ya kuweka hofu zangu kando sikuwa na budi ila kuimba
vilivyo na kufurahia huo wakati.
SWALI: Ni wasanii gani humu nchini na mbali ambao ungetamani sana kufanya kazi nao?
JIBU: Tangu zamani nilitamani kufanya kazi na Collo, ndoto ambayo ilitimia kupitia kibao, 'Milele'. Ningependa sana kushirikiana na Juliani na malkia wa repa, STL. Nje ya Kenya, ningependa sana kufanya kazi na Ali Kiba, Tiwa Savage, vile vile Mafikizolo.
SWALI:Changamoto yako kuu kimuziki imekuwa gani?
JIBU: Tatizo langu kuu limekuwa suala nyeti ambalo limekuwa likiathiri muziki wa Kenya, kutopata mwangaza wa kutosha kimuziki.

Ikiwa muziki wa nje utapewa mwangaza mwingi zaidi ya utunzi wa Kenya bila shaka inaendeleza dhana kuwa muziki wa Kenya haujaboreka vya kutosha.

Ni tatizo ambalo limezidi kurudisha nyuma sekta ya muziki nchini.