http://www.swahilihub.com/image/view/-/2605138/thumbnail/932825/-/hxfgxk/-/shanton+flv.jpg

 

Shanton: Mie ni msanii na afisa wa polisi

Na  PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Wednesday, January 28  2015 at  17:28

Kwa Muhtasari

Licha ya hatari na ugumu wa kuwa askari wa kupambana na wizi wa mifugo katika eneo la Turkana, bado ana muda wa kutunga nyimbo, kipaji alichokitambua akiwa katika shule ya chekechea.

 

LICHA ya hatari na ugumu wa kuwa askari wa kupambana na wizi wa mifugo katika eneo la Turkana, bado ana muda wa kutunga nyimbo, kipaji alichokitambua akiwa katika shule ya chekechea.
Huenda hiyo ndio ilikuwa sababu iliyompa Antony Bosiben al-maarufu Shanton ujasiri wa kumuandikia na kumtumia malkia wa muziki, Rihanna wimbo miaka sita iliyopita akiwa katika kidato cha pili.
Kibao hicho kwa jina 'Cosy Lifestyle' kilinuiwa kutambua mafanikio ya Rihanna katika ulingo wa muziki kimataifa, halikadhalika maisha yake ya hali ya juu.
“Nilitumia kampuni ya muziki ya Def Jam maneno kamili ya wimbo huo kupitia barua pepe. Sina uhakika iwapo wimbo huu ulimfikia lakini nina matumaini kuwa wakati mmoja atasikia sauti yangu,” aeleza.
Mtindo wa Shanton wa muziki unahusisha mchanganyiko wa repa ya kawaida, rock pamoja na kapuka, mtindo anaosema kuwa haujashuhudiwa miongoni mwa wasanii hapa nchini.
Asema ari yake ya kuwa mwanamuziki ilichangiwa na mamake ambaye alikuwa muimbaji wa injili.

“Hata hivyo kama msanii hakupata fursa ya kurekodi kibao chochote kutokana na ugumu wa sekta ya muziki wakati huo,” aeleza.
Kipaji chake kimuziki kiliota hata zaidi akiwa katika shule ya upili ya Cheptoroi, eneo la Njoro ambapo wakati mmoja alipokea taji la kuwa mwanarepa bora katika shindano la kumtafuta mwanamuziki shupavu.
Ni hapa ndipo alipewa jina Shanton ambalo ni ufupisho wa 'Shy Antony', jina alilopokea akiwa shuleni, kutokana na  uoga wake.
Kufikia hapa nia yake ya kuwa mwanamuziki ilikuwa thabiti na baada ya kukamilisha masomo aliamua kukutana na madijei fulani wa kampuni ya muziki ya Ogopa kupitia mtandao na kuanzisha rasmi safari yake kimuziki.
Hata hivyo ilimbidi kusubiri kwa muda kwani alirekodi kibao chake cha kwanza “Red Carpet” mapema mwaka huu, pindi bada ya kuhitimu kutoka chuo cha mafunzo ya GSU.

Kibao kinapaa
“Kibao hiki kinfanya vyema kwani tayari kinachezwa katika baadhi ya vituo vya redio na televisheni,” adokeza.
Kwa sasa anafanyita kazi video yake mpya “Tell em” huku akiwa na mipango ya kuizindua January mwaka ujao“Imekamilika lakini sharti nisubiri ili nizindue audio na video pamoja,” aongeza.
Kati ya changamoto ambazo zimekuwa zikimuumisha mbali na ukosefu wa pesa za kutosha kurekodi muziki, analalamikia suala la wakati.

“Kama afisa wa polisi kazi huwa nyingi  ambapo wakati mwingine nahitajika kurekodi wimbo, ilhali ni zamu yangu ya kulinda usalama,” aeleza.
Pia anasema suala la usalama limekuwa changamoto.

“Kuna wakati ambapo pengine nahitajika kuja Nairobi kurekodi muziki au kufanya shoo, lakini kutokana na hatari katika maeneo haya inanibidi kuhairisha mipango yangu,” aeleza.

Shida ya maprodusa
Pia kuna shida ya kupata maprodusa bora kwani wanasanii wengine huishia kuharibu pesa baada ya kurekodi nyimbo katika maprodusawasiojua kazi.
Lakini anasema hii ni kawaida kwani kama mwanamuziki sharti ukumbane na shida hizi kuashiria kuwa uko hai katika sekta hii.
Japo anakiri kuwa yungali mbichi katika muziki na hivyo hajawahi tambuliwa popote, Shanton anasema kuwa matumaini yake ya kutia alama hasa kuanzia mwaka yako thabiti.
“Najiona sio tu kama nyota hapa barani bali pia ulimwenguni kote na ili kuafikia hayo, pia napanga kuandaa mahojiano na wanahabari kila mara angalau nijiuze kama mwanamuziki,” aeleza.
Ndoto yake inasalia kushirikiana na Octopizzo, vile vile Rihanna na Jay Z katika ngazi ya kimataifa.
Mbali na kuwa mwanamuziki yeye pia ni mwandishi wa vipindi na mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano.