http://www.swahilihub.com/image/view/-/2605180/thumbnail/932851/-/7n3a87/-/Gola+flv.jpg

 

Golikipa wa Mathare United anayeazimia kuidakia mpira Barcelona

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Wednesday, January 28  2015 at  18:06

Kwa Muhtasari

Kwa mwaka mmoja sasa ni amekuwa golikipa nambari mbili wa klabu ya Mathare United, timu aliyoanza kuichezea mwezi Mei mwaka jana.

 

KWA MWAKA mmoja sasa ni amekuwa golikipa nambari mbili wa klabu ya Mathare United, timu aliyoanza kuichezea mwezi Mei mwaka jana.
Licha ya muda huu mfupi ambao Peter Odhiambo amechezea klabu hii, amefanikiwa kushiriki katika mechi saba na kuisaidia timu yake kumaliza ya kumi katika ligi ya kitaifa ya primia msimu uliopita.
Lakini hii haimaanishi kuwa nyota yake ilianza kung’aa akiwa katika timu hii, kwani hata kabla ya hapa kipaji chake kama golikipa kilikuwa kimejitokeza.
Kati ya 2008 na 2009 alichezea timu ya taifa ya wavulana wasiozidi miaka 17 katika kombe la Copa Coca Cola nchini Afrika Kusini.
Mwaka mmoja baadaye alishiriki katika kombe la CECAFA nchini Sudan na hata kuteuliwa kama golikipa bora.

“Pia wakati huo huo nilishiriki katika mchuano wa kirafiki nchini Ethiopia,” aeleza.
Kadhalika katika msimu huo pia, alishiriki katika mashindano ya kufuzu kwa Kombe la dunia kwa vijana wasiozidi miaka17, nchini Djibouti.
Mwaka wa 2011alijumuisha kikosi cha timu ya taifa iliyoshiriki katika mashindano ya wavulana wasiozidi miaka 18 yaliyoandaliwa Umbrae nchini Italia.

“Hapa tulifanya vyema na kumaliza wa pili baada ya kuibwaga Uingereza katika nusu fainali, na hatimaye kuangushwa na Italia.
“Pia mwaka huo tulishiriki katika mashindano ya wavulana wasiozidi miaka 20 katika shindano la Nile Basin jijini Cairo, Misri na hata kufuzu kwa michezo ya Olimpiki kwa wavulana wasiozidi miaka 23 dhidi ya Rwanda.
Kama wanasoka wengi ulimwenguni kipaji chake kilianza akiwa mdogo na kama mwanafunzi wa shule ya msingi ya Makongeni hapa jijini Nairobi, tayari alikuwa ameanza kung’aa na hata kujumuishwa katika kikosi cha shule.
Hata hivyo kutokana na ukosefu wa karo hakufanikiwa kujiunga shule ya upili, lakini hilo halikumaanisha kuwa nyota yake kama mwanasoka ilikuwa imezima.
Katika umri mdogo wa miaka kumi na miwili tayari alikuwa ameanza kuonyesha umahiri uliompelekea kujumuishwa katika kikosi cha klabu ya Dandora, kwa vijana wasiozidi miaka 12.
Mwaka wa 2008 akiwa hapa alijiunga na klabu ya Petra Boys, kikosi cha chipukizi cha timu ya City Stars, alikocheza kwa mwaka mmoja kabla ya kujiunga na kikosi cha watu wazima cha timu hiyo.

“Hapa nilicheza hadi nilipojiunga na timu yangu ya sasa, mwaka jana,” aongeza.
Changamoto ambayo imezidi kumkabili kama wachezaji wengine ni kutopata muda wa kufanya mazoezi, pamoja na majeraha ya kila mara ambayo huathiri uchezaji.
Lakini hilo halijazima ndoto yake ya wakati mmoja kuchezea timu ya taifa, Harambee Stars.

Pia japo anafurahia kuichezea Mathare United, azma yake ya siku za usoni inasalia kujumuishwa katika kikosi cha Barcelona, nchini Uhispania.