http://www.swahilihub.com/image/view/-/2708624/medRes/1007682/-/vi24e2z/-/BDMPESA0412Z.jpg

 

Safaricom yavuna Sh3.1 bilioni kutokana na 'Okoa Jahazi'

Bob Collymore

Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom Bob Collymore akihutubu awali. Picha/DIANA NGILA 

Na GEORGE NGIGI

Imepakiwa - Monday, August 15  2016 at  17:30

Kwa Muhtasari

Wateja wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom walikopeshwa kiwango cha muda wa mawasiliano ya simu kisichopungua Sh30 bilioni mwaka uliopita.

 

WATEJA wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom walikopa kiwango cha muda wa mawasiliano ya simu kisichopungua Sh30 bilioni mwaka uliopita.

Mkopo huo ambao hutolewa kupitia kwa huduma ya 'Okoa Jahazi’ hugharimu wateja asilimia 10 ya kiwango wanachokopesha, na hivyo basi Safaricom ikapata faida ya Sh3.1 bilioni katika huduma hiyo.

Katika mahojiano ya awali na gazeti la Business Daily linalomilikiwa na kampuni ya Nation Media Group, aliyekuwa Afisa Mkuu wa Fedha katika Safaricom Bw John Tombleson alisema Okoa Jahazi huwaletea asilimia 28 ya jumla ya mapato yao.

Katika kipindi cha kifedha kilichokamilika Machi mwaka huu, mapato ya Safaricom yalifika Sh90.8 bilioni, kutoka Sh87.3 bilioni mwaka uliotangulia.

Mwaka uliopita, kulikuwa na asilimia 250 ya wateja waliokopesha muda wa mawasiliano ya simu na hawakulipa madeni hayo kwa wakati unaofaa. Kiwango walichokuwa wameomba kilikuwa Sh705 milioni.

Kutokana na msingi kuwa wateja wako radhi kutozwa asilimia 10 ya kiwango wanachoomba, ni ishara kuwa wengi wao huwa hawana namna nyingine ya kununua muda wa mawasiliano ambayo imekuwa muhimu kwa wananchi wengi.