Vipengele muhimu katika uchanganuzi wa maana katika Kiswahili

Na MARY WANGARI

Imepakiwa - Saturday, September 9  2017 at  19:38

Kwa Mukhtasari

Katika makala iliyopita tulianzisha uchambuzi wa mada kuhusu maana ya kimsingi ya dhana ya semantiki katika Kiswahili.

 

KATIKA makala iliyopita tulianzisha uchambuzi wa mada kuhusu maana ya kimsingi ya dhana ya semantiki katika Kiswahili.

Tuliangazia vipengele mbalimbali ikiwemo ishara anuai za maana.

Katika mada ya leo tuajikita zaidi katika uchambuzi wa maana katika semantiki jinsi ifuayavyo:

NYANJA KUU ZA KUCHANGANUA MAANA YA MAANA
Maana ya maana huchanganuliwa katika nyanja kuu mbili kama ifuatavyo:
1) Maana ya msingi
2) Maana ya ziada.

Maana ya Msingi (Maana ya Kileksia)

Hii ndiyo maana kuu ya neno, maana hii haibadiliki kwa kutegemea mabadiliko ya mazingira au athari za mazingira.

Fahiwa (sense) nyingine zote za maana zinazohusiana huibuka kutokana na maana ya msingi. Maana ya msingi pia huitwa maana ya kilekisia. kwa mfano

i. kupe – mdudu anyonyaye damu
ii. mrija- kifaa cha kupitishia kitu kiowevu kuelekea kwenye chombo kingine
iii. funika- zuia kitu ili kisionekane kwa kutumia kitu kingine kama kifuniko, nguo na kadhalika

Maana ya Ziada (Maana ya Kisarufi)
Ni maana ambazo huibuka kutokana na maana za msingi. Maana hizi huhusiana na muktadha. Uelewekaji wake hutegemea muktadha ambamo neno linatumika.

Kama jina lenyewe linavyodokeza, maana ya ziada ni ziada ya maana ya kawaida/msingi.
Kwa mfano
i. bosi wetu amekuwa kupe siku hizi(mnyonyaji)
ii. hatuwezi kupiga hatua kama taifa iwapo hatutakata mirija yote (ufisadi/ rushwa)
iii. katika tuzo kuu la mwaka jana Ali Kiba alimfunika Diamond (alimshinda)

Hata hivyo maana ya msingi na maana ya ziada zinahusiana kwa karibu sana kwani maana ya ziada hutokana na maana ya msingi.

Aina za Maana
Wataalam wengi mathalan Leech (1981) wanakubaliana kuwa kuna maana saba (7) kama ifuatavyo;


i. Maana ya Msingi

ii. Maana Dokezi

iii. Maana Mtindo

iv. Maana Hisia

v. Maana Tangamani

vi. Maana Mwangwi

vii. Maana Dhamira

MAANA YA MSINGI (DENOTATIVE MEANING)
Hii ndiyo maana kuu ya neno ambayo haibadiliki kutokana na mazingira.
Maana nyingine zote za ziada ambazo zinahusiana hutokana na maana hii ya msingi.aina hii ya maana huangaliwa na kufafanuliwa kwa kigezo cha kuwapo au kutokuwapo kwa sifa bainifu (distinction features) zinazokibainisha kitu hicho.

Sifa hizo baininifu katika taaluma ya semantiki huitwa vijenzi semantiki
Kwa mfano maana ya neno mwanamke linasheheni sifa bainifu zifuatazo::
+mtu
+mtu mzima
+ke
-me
Neno mwanamume nalo linasheheni sifa hizi bainifu:
+mtu
+mtu mzima
+me
-ke

MAANA DOKEZI (CONNOTATIVE MEANING)
Hii ni maana ambayo hudokezwa na kile kisemwacho na kuwakilishwa na kinachorejelewa na lugha.

Maana hii inapatikana kwa njia ya kitu fulani kuwakilisha au kudokeza kitu fulani kingine au hali nyingine.

Maana dokezi hutokana au huibuliwa na sifa tatu kuu zifuatazo:

Sifa za umbo la kitu
Hapa kinachoangaliwa ni umbo la kile kitu.
Umbo hilo huchukuliwa kukitofautisha na kitu kingine.

Kwa mfano:
Mwanamke +matiti
+ujauzito
+miondoko

ii) Sifa za kisaikolojia (mtu mwenyewe anavyojichukulia)
Katika kipengele hiki kinachoangaliwa zaidi ni ile hali ya kile kitu kisaikolojia (kwa ndani zaidi) au ukipenda hisia.
kwa mfano:
Mwanamke. + huruma
+ Upendo
iii) Mtazamo wa watu kuhusu kitu hicho.
Unahusu mtazamo wa watu wengi kuhusu kitu hicho.
Kwa mfano jamii inaamini kwamba:-
Mwanaume +Jasiri
+nguvu na kadhalika

Hivyo basi maana hizi zote zinategemea muktadha wa usemaji.
Maneno haya yakiwa pwekepweke huwezi kuyatolewa maana iliyokusudiwa.

MAANA YA KIMTINDO (STYLISTIC MEANING)
Maana hii huhusiana na muktadha wa matumizi ya lugha. Mitindo hiyo ni pamoja na:
1. Mitindo ya kilahaja,
2. Mitindo ya kiwakati,
3. Mitindo ya kieneo/kitaaluma/fani fulani.
4. Mfano ‗fahamu‘ ,
5. Mitindo ya kiuwasilishaji,
6. Mitindo ya kihadhi na
7. Mitindo ya binafsi

MAANA HISIA (EFFECTIVE MEANING)
Maana hii inategemeana na inahusiana na hisia na mtazamo wa msemaji au mwandishi.
Aidha, maana hii huwakilishwa kwa njia nyingi.
Baadhi ya njia hizo ni kwa kutumia maana ya msingi/dokezi.
Kwa mfano ‗wewe ni mwanaume kweli kweli kwa maana kwamba wewe ni jasiri, shujaa na kadhalika.
Au acha kulialia kama mwanamke bwana!
Kwa kutumia njia isiyo ya moja kwa moja.
Kwa mfano ‗hongera, naona leo umewahi kweli kweli‘
-huku akimaanisha amechelewa(kejeli)

Maana hisia mara nyingi hubadilika kutegemea kiimbo hata kama maneno ni yale yale.

Kwa mfano neno 'mpole'

MAREJEO
Habwe, J. na Karanje, P. (2004) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, Phoenix Publishers Ltd. Nairobi-Kenya.

TUKI (2004) Kamusi ya kiswahili sanifu, Oxford University press, Dar es Salaam.

Una swali ungependa kupata jibu lake? Muulize mwandishi kupitia anwani:marya.wangari@gmail.com