Waliokabidhiwa dhamana ya Kiswahili wawe na  mtazamo mpya

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Thursday, November 2  2017 at  14:45

Kwa Mukhtasari

Ziko hatua ambazo zimechukuliwa na viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kukienzi Kiswahili.

 

ZIKO hatua ambazo zimechukuliwa na viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kukienzi Kiswahili.

Hatua ya kwanza iliyochukuliwa na viongozi wetu  baada ya kuanzishwa upya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1999 ni kukubali kuanzishwa kwa Tume ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Tume hii ilipewa dhima ya kukuza, kuratibu, kuendeleza, kuwahamasisha wananchi kukitumia Kiswahili katika mazingira mbalimbali kama kwenye mikutano, warsha, semina na mawasiliano ya kibiashara na kiuchumi.

Walikubaliana kwamba matumizi yawe kwa uwiano ulio sawa katika tahajia pamoja na matamshi na mpangilio wa maneno katika sentensi.

Kwa hiyo waandishi wa vitabu na magazeti watatakiwa kuzingatia mfumo wa uandishi uliokubalika katika nchi wanachama. Hali kadhalika imetakiwa matamshi ya maneno kwa watangazaji katika redio na runinga yawe sahihi na yasiathiriwe na lugha zao za asili.

Mfano mzuri wa kuigwa ni katika  lugha ya Kiingereza inayotumika katika matangazo ambapo watangazaji wanapata mwongozo wa matamshi bora ya lugha yaliyokubalika. Mfano mzuri unaofahamika ni mtindo wa lugha unaojulikana kama ‘RP au Queen’s English.’ Mtindo huu unazingatia matamshi yanayokubalika na ndiyo unaomfanya mzungumzaji au mtangazaji kwenye redio na runinga asijulikane kama anatokea Wales, Scotland au jijini London ambako iko lahaja inajulikana kama ‘Cockney’ yenye lafudhi ya kipekee. Kwa hiyo lahaja hii haitumiki katika matangazo rasmi au katika uandishi.

Kwa upande wa Kiswahili, upotoshaji wa matamshi na tahajia yake unaweza kuepukwa kama kungekuwapo na mitalaa ya safuri inayofanana katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya uandishi wa habari katika nchi zetu za Jumiya ya Afrika Mashariki.

Wakoloni walitambua tatizo hili na ndiyo maana waliunda Kamati ya Lugha ya Kiswahili ya Afrika Mashariki iliyoshughulikia  masuala haya kwa mapana yake. Hata hivyo hawakufanikiwa sana kwani wajumbe wa kamati hii tangu mwanzo walikuwa ni Wazungu ambao hawakuwa na misingi imara ya lugha ya Kiswahili. Waafrika wachache walianza kushirikishwa kwenye miaka ya 1939 lakini bado idadi ya Wazungu ilikuwa kubwa kuliko ya Waafrika.

Tangu mwaka 1964 kila nchi za  Afrika Mashariki ilikuwa huru na hivyo kuamua kuwa na sera ya lugha iliyokubalika katika nchi hizi.

Hali ilianza kuwa mbaya na kuanza kuwa na Kiswahili cha Kenya, cha Zanzibar na cha Tanzania Bara. Huu mtafaruku unaoendelea  hadi sasa na unatakiwa kupigwa vita ili kuuondoa.

Ni matumaini yangu kuwa vyombo vyenye dhima ya kukuza na kuendeleza Kiswahili vitajizatiti kupambana na upotoshaji unaojitokeza.

Wataalamu wa lugha kwa nchi  wanachama waliopo katika taasisi, asasi za lugha, kampuni za uchapishaji vitabu na watu binafsi  wa nchi za  Jumuiya ya Afrika Mashariki na wale wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako Kiswahili kinatumika wakutanishwe ili kupata mwafaka.

Lengo ni kuifanya lugha inayotumika katika redio, runinga, magazeti na pia shuleni katika nchi hizi ikubalike.

Kwa sasa Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ambayo ilizinduliwa rasmi tarehe 6 hadi 8 Septemba 2017 makao yake makuu yako  Zanzibar.

Mada kuu wakati wa uzinduzi wake ilikuwa ni “Kuleta Mabadiliko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutumia Kiswahili". Swali la kujiuliza ni  je, ni nini kipaumbele cha Tume hii mara baada ya kupata fedha za kutekeleza miradi yake kulingana na shabaha zilizowekwa? Ni muhimu programu mahususi ziandaliwe mapema na kuanza kupambana na changamoto zinazokikabili.

Viongozi walioteuliwa kuongoza Tume hii waanze kupanga programu za utekelezaji baada ya kupata ushauri na mapendekezo kutoka kwa wadau wa Kiswahili.

Wadau hawa ni walimu na wahadhiri wa Kiswahili, waandishi na wachapishaji vitabu, watafiti wa taasisi na asasi zinazojishughulisha na Kiswahili.

Nchi za Kenya, Tanzania na Uganda zina uzoefu mkubwa tangu enzi za ukoloni. Wadau wa nchi hizi washirikishwe wakiwamo wenyeji wa Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Komoro.

Ushauri wangu ni kuwa wataalamu wasikubali kukaa kitako kwenye warsha au semina na kuanza kupanga mipango ya lugha wakiwa peke yao bila kuwa na ushirikishwaji mpana wa watu wa mashinani/vijijini ambao ni watumiaji wakubwa wa Kiswahili.

Wataalamu wa Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki walifanya makosa wakati wa kukisanifu Kiswahili. Hawakuwashirikisha wenyeji wa lugha hii na matoleo yake ni kuipotosha kwa lugha hii katika baadhi ya tahajia za maneno kama  kuona/kuonya, tofauti /tafauti na kadhalika.

Pia katika mpangilio wa maneno katika sentensi  kama shangazi yangu/shangazi langu), mfereji wa maji/bomba la maji na kadhalika.

Umefika wakati tuanze kujifunza kutokana na makosa haya, ili tuyarekebishe na tusonge mbele kwa kuzingatia misingi ya lugha.

Misingi hii itaimarishwa kwa kutunga sera ya lugha ya Kiswahili inayoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Nambari za Simu: 0754 861664, 0716 694240