http://www.swahilihub.com/image/view/-/3488614/medRes/1513923/-/44unypz/-/idrissa.jpg

 

Washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell watangazwa

Idrissa Haji Abdalla

Idrissa Haji Abdalla (Tanzania) wa Kilio cha Mwanamke. Picha/HISANI 

Na HEZEKIEL GIKAMBI

Imepakiwa - Friday, December 16  2016 at  11:17

Kwa Mukhtasari

Washindi wa mkumbo wa pili wa shindano la Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika inayotambua kazi za waandishi wa Kiswahili pekee, tena kutoka eneo zima la Maziwa makuu, wametangazwa.

 

WASHINDI wa mkumbo wa pili wa shindano la Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika inayotambua kazi za waandishi wa Kiswahili pekee, tena kutoka eneo zima la Maziwa makuu, wametangazwa.

Washindi hao wa mwaka 2016 walitangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Abdilatif Abdalla, tarehe 14 Disemba, 2016.

Zawadi za Tuzo hii zitatolewa Tanzania katika Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, Kilimanjaro, Ukumbi wa Kibo, tarehe 16 Januari, 2017.

Washindi wa mwaka 2016 ni:

Riwaya

  1. Idrissa Haji Abdalla (Tanzania), Kilio cha Mwanamke ($5,000)
  2. Hussein Wamaywa (Tanzania), Moyo Wangu Unaungua ($3,000)

Ushairi

  1. Ahmed Hussein Ahmed (Kenya), Haile Ngoma ya Wana ($5,000)

Kama ilivyotangazwa kabla, wafuatao ni waandishi wengine waliokuwamo katika orodha fupi:
 Ally Hilal (Tanzania), Mmeza Fupa (riwaya)
 Hussein Wamaywa (Tanzania), Mkakati wa Kuelekea Ikulu (riwaya)
 Richard Atuti Nyabuya (Kenya), Umalenga wa Nyanda za Juu (ushairi)

Shindano hilo lilizinduliwa jijini Nairobi Disemba 2014, na Dkt. Lizzy Attree (Mkurugenzi wa Tuzo ya Caine) na Dkt. Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell) na linaendeshwa kwa udhamini wa kampuni ya Mabati Rolling Mills na Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani.

Meneja wa Masoko wa Mabati Rolling Mills Bw Harry Njagi, wakati wa uzinduzi huo alisema kwamba lengo hasa ni kurejesha shukrani kwa watu wa eneo la Maziwa Makuu, ambao wamenufaika pakubwa na wamekuwa wateja wa dhati wa bidhaa za mabati na paa za nyumba kwa jumla.

“Kampuni hii iko katika mataifa 18 ya Afrika. Kati ya mataifa hayo, Kiswahili kinazungumzwa Kenya, Uganda, Tanzania, DRC, Sudan Kusini, Rwanda na Burundi. Tunajua kwamba Kiswahili ndiyo lugha nyepesi inayotumika tunapowasambazia bidhaa zetu,” akasema Bw Njagi.

Meneja wa Uhusiano mwema Bw Salim Bakari, alisema shindano hilo ni la kuendeleza na kukuza utamaduni, mila na lugha ya Kiswahili, ambayo haijatambuliwa sana kupitia tuzo.

Ni shindano linaloangazia kunga mbili kuu za uandishi wa Kiswahili - Hadithi na Mashairi.

Kwa habari zaidi kuhusu Tuzo hii, tazama: http://kiswahiliprize.cornell.edu